• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wanaume wawili kusalia ndani kwa kunajisi mabinti

Wanaume wawili kusalia ndani kwa kunajisi mabinti

Na RICHARD MUNGUTI

WANAUME wawili walioshtakiwa kwa kuwanajisi binti zao watasalia gerezani hadi korti itakapoamua kesi dhidi yao huku jumla ya wanaume watano wakishtakiwa kwa makosa ya dhuluma za kimapenzi.

Washtakiwa walikabiliwa na madai ya kunajisi na kuwadhulumu wasichana wa umri mdogo kwa kuwatia vidole katika nyeti zao kinyume cha sheria.

Kati ya watano hao ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Kenyatta.Alishtakiwa kumdhulumu kimapenzi msichana mwenye umri wa miaka 15 , Kasarani Nairobi.

Kina baba hao wawili walio na umri wa miaka 45 kila mmoja waliagizwa na hakimu mwandamizi mahakama ya Kibera Nairobi Bw Charles Mwaniki Kamau wazuiliwe gerezani wasiwatishe walalamishi wakose kufika kortini kueleza masaibu waliyopitia mikononi mwa baba zao.

“Ninyi mtasalia gerezani hadi kesi zinazowakabili zisikizwe na kuamuliwa.Mko na uhusiano wa baba na binti na mkiachiliwa mtawatisha wasije kortini kutoa ushahidi dhidi yenu,” Bw Kamau aliwaeleza wawili hao (Samson Ombeyi Ongachi na Alex Vudukhu Luvanda) akitoa maelekezo.

Walikanusha shtaka la kuwadhulumu kimapenzi walalamishi katika mitaa ya Kibera, Embakasi na Kasarani kaunti ya Nairobi.

Alex Vudukhu Luvanda.

Bw Kamau alitoa agizo hilo baada ya kuelezwa na kiongozi wa mashtaka Bw Geoffrey Obiri kwamba “visa vya dhuluma za kimapenzi zimesheheni katika mitaa mbali mbali Nairobi na hatua kali yahitaji kuchukuliwa dhidi ya wahusika iwe funzo kwa wengine.”

“Naomba hii mahakama ichukulie suala hili la baba kumnajisi ama kumdhulumu kimapenzi bintiye kwa uzito mno,” alisema Bw Obiri.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema wasichana wamo hatarini na watapata afueni tu iwapo hatua kali zitatchukuliwa dhidi ya washukiwa wanaofikishwa kortini.

Pia alisema masharti makali ya dhamana yatatolewa na mahakama.

“Naomba hii mahakama ianze kuchukua hatua kali kwa washukiwa wa ubakaji , dhuluma za kimapenzi dhidi ya wasichana na wavulana wanaolawitiwa,” Bw Obiri alisema.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema ni jukumu la kina baba na wanaume waliohitimu umri wa zaidi ya miaka 18 kuelewa jukumu lao ni kuwatunza wasichana na kina mama na wala sio kuwadhulumu kimapenzi.

Kina baba hao (Samson Ombeyi Ongachi na Alex Vudukhu Luvanda) walikana mashtaka dhidi yao na kueleza mahakama “ ni kuonewa tu.”

Kwa masikitiko mmoja wao (vudukhu) alimweleza hakimu, “Mimi nimeonewa kabisa. Nitawezaji kumnajisi binti yangu.Atakapofika kortini ukweli utajulikana. Hizi ni njama kati ya Daktari na mlalamishi na ukweli utakithiri ushahidi ukiwasilishwa.”

Baba huyo alieleza korti itenge siku ya karibu kesi isikizwe na kuamuliwa ndipo ajinasue na kesi inayomkabili.

Washukiwa watatu walioshtakiwa kuwadhulumu wasichana kimapenzi waliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.

Walioshtakiwa ni Ongachi, Vudukhu, Geoffrey Orogo Gesicha, Jason Ambalo Mutuli na Cyrus Thairu Maina.

Kesi dhidi ya washtakiwa hawa zitatajwa Agosti 31 2020 kwa maagizo zaidi.

Bw Obiri aliamriwa awape washukiwa nakala za mashahidi waandae tetezi zao.

  • Tags

You can share this post!

Washtakiwa kuiba maziwa

Akana kutandika wawili mtaani Tassia