Habari Mseto

Wanawake waonywa dhidi ya kuwatwanga waume zao

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY KIMATU

WANAWAKE wameombwa kukoma kuwatwanga waume zao nyumbani kuhusu misukosuko katika ndoa.

Badala yake wameshauriwa kuwatii waume wao kama inavyofundisha Biblia Takatifu na kuwauliza wazazi kupeleka watoto wao katika kongamano za makanisa au jandoni hasa wakati huu wa likizo ndefu ya Disemba..

Hayo ni kulingana na mwanzilishi na mkurugenzi wa shirika la Visionary Naomiruth Women, Bi Emma Murunga.

“Ni muhimu kwa mwanamke kujifunza kuwekeza pamoja na kusimamia mambo ya nyumba au boma kupitia mafunzo ya kiroho. Wanawake komeni kupiga mabwa wenu na badala yake muwe watiifu kwani ni sharti mwanamume awe kichwa pale nyumbani. Wazazi pelekeni wanao makanisani, misikitini na jandoni badala ya kuwaacha watoto wakirandaranda masokoni na barabarani,” Bi Murunga akanena.

Alikuwa akiongea wakati wa kuadhimisha mwaka mmoja sawia na kufuzu kwa mahafala wa kike waliofundishwa masuala ya kujiinua kupitia mafunzo ya kiroho, kiuchumi, kijamii na jazba.

Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika kanisa la Reconciliation Christian Centre ilioko katika mtaa wa Jericho, Kaunti ya Nairobi.

Washiriki walimuwa ni wanawake kutoka Kaunti 21 hapa nchini Kenya na wengine kutoka ng’ambo ikiwemo wa Libya, Egypt, Iran, Iraq na Bahrain.

Wanawake hao walipatikana kupitia mawasiliano ya mitandao ya jamii ya Whatsapp na telegram wakiwasiliana kupitia kwa rununu.

Kadhalika, Bi Emma aliwakumbusha wakristo kuiombea serikali na kuongeza kwamba ni jukumu la kanisa kufanya hivyo kulingana na Biblia.

Waliofuzu walitunukiwa vyeti na shirika hilo kuongeza kwama inalenga kufikia kaunti zilizobakia 26 ifikapo Mwaka 2020.