Wanawake wataka ulinzi dhidi ya mabichi-boi
Na FARHIYA HUSSEIN
WANAWAKE mjini Mombasa sasa wanataka polisi wawalinde dhidi ya wanaume wanaowadhulumu kwenye fuo za bahari nyakati za sherehe kama hii ya Pasaka.
Wanasema wanaume hao mabichi-boi wanaojifanya kuwa wanaowafunza kuogelea, mara nyingi huwageukia na kuwalazimisha kushiriki nao tendo la ngono.
Baadhi ya waliozungumza na Taifa Leo walisema wanaume hao, wengi wakiwa wafanyibiashara wa maduka madogo yaliyoko fuo za bahari, hutumia fursa za kuwasaidia mabinti kuogelea na kuwatomasa.
Uchunguzi wa Taifa Leo ulionyesha idadi kubwa ya wanawake hao na wasichana huvumilia uovu huo, kwa kuogopa kuzamishwa baharini.
Mmoja wao ambaye tutamwita Mary kwa sababu za usalama wake na kumlinda, alisema wakati mmoja alienda kuogelea baharini na akajikuta akilazimishwa na mtu aliyekuwa amemuamini kuwa angemsaidia kuogelea.
“Nilienda hapo na mmoja wa wale vijana akajitolea kunisaidia kuogelea. Lakini tulipofika ndani ya bahari alinigeukia. Alitaka tushiriki kitendo huko majini, la sivyo aniachilie nife maji,” akalalamika Bi Mary.
Alieleza kuwa wanawake wengi huwa wanakubali wanapoambiwa ni mafunzo ya kuogelea pekee ilhali hawajui pindi wanapokubali mafunzo hayo, mwishowe hugeuka na kuwa ubakaji.
“Mara nyingi huwa wanaangalia yule ambaye ni mgeni katika eneo hilo na kutumia lugha tamu za kumtongoza. Anapokubali, huenda naye hadi kwenye maji ambapo mtu hawezi kukanyaga chini bila kufa maji. Ndipo wanapofanya unyama huo,” akasema.
Apiga usiahi
Mwingine tunayemtambua tu kama Mama Janice, alieleza jinsi wakati mmoja alijaribu kupiga kelele ili kujiokoa lakini hakujinasua.
“Nakumbuka wakati nilikwenda baharini jamaa mmoja alinieleza angenisaidia kuogelea ili nisizame majini na niwe na wakati mzuri. Tukiwa majini, nilikataa kuendelea kwenda katikati ya bahari, lakini alinilazimisha na baadaye akanibaka.”
Alieleza kuwa alimshtaki kwa mumewe lakini hakumuamini na kusema yeye mwenyewe ndiye aliyejipeleka mikononi mwa vijana hao.
Kutokana na kuongezeka kwa visa hivyo, sasa wanawake hao wanamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw Hillary Mutyambai, atume vikosi vyake kuwapiga msasa wanaofanya biashara ya kufunza watu kuogelea katika fuo za umma.
“Kuna Polisi wa Fuo za Bahari wanaolinda watalii. Kwa nini sisi tunaotembelea fuo hizo hatuchukuliwi kuwa watalii na kulindwa dhidi ya unyama huu?” aliuliza mmoja wa wanawake hao.