Habari Mseto

Wandani wa Ruto wataka ICC iingilie

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na NICHOLAS KOMU

MALUMBANO yaliendelea kushamiri Jumatatu kuhusu fujo zilizozuka Jumapili wakati wa ziara ya Naibu Rais William Ruto katika eneo la Murang’a huku wabunge wa mrengo wa Tangatanga wakiitaka Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) kuingilia kati na kuchunguza ghasia hizo.

Watu wawili walifariki katika ghasia hizo pale wafuasi wa Dkt Ruto walipokabiliana na wale wa kundi pinzani la Kieleweke waliojaribu kumzuia kuendesha hafla ya kuchanga pesa katika kanisa la AIPCA mjini Kenol.

Jumatatu, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga alilaani fujo hizo huku akionya Naibu Rais na wabunge wa mrengo wake dhidi ya kuanza kampeni za mapema za urais, miaka miwili kabla ya mwaka wa 2022.

“Hayo machafuko na uharibifu wa mali yaliyotokea Murang’a wakati wa kampeni za urais yanawatia hofu Wakenya na yanafaa kulaaniwa vikali,” Bw Odinga akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Aliitaka serikali kuchukua hatua za haraka na kuchunguza ghasia hizo kwa lengo la kuwaadhibu waliochochea fujo hizo.

Wito sawa na huo ulitolewa na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ambayo ilizitaka asasi za usalama na zile za upelelezi kuwasaka na kuwakamata wale ambao walichochea vijana kuzua fujo.

“Na kwa vijana wetu tunawashauri kukoma kutumiwa vibaya na wanasiasa na watu wengine wenye nia mbaya katika jamii. Fujo si suluhu kwa changamoto zinazolikabili taifa hili wakati huu,” akasema mwenyekiti wa tume hiyo Dkt Samuel Kobia.

Lakini wabunge wa Tangatanga walielekeza kidole cha lawama kwa serikali wakidai ndiyo iliyodhamini machafuko hayo na kuyafanikisha kwa kutumia polisi.

“Tunataka kusema hapa kwamba fujo ambazo zilishuhudiwa kule Murang’a zilichochewa na kufadhiliwa na Serikali. Hii ndiyo maana polisi walitumiwa kurusha vitoa machozi ndani ya kanisa na hivyo kuchafua nyumba ya Mungu,” akasema Mbunge wa Kikuyu, Bw Kimani Ichung’wa jana kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

Aliongea kwa niaba ya wenzake saba, alioandamana nao, akiwemo Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.

“Hii ndiyo maana tunataka Kenya na mahakama ya ICC kuingilia suala hili kwa sababu tunaamini ghasia kama hizi zinalenga kuvuruga uchaguzi mkuu wa 2022. Tunataka ICC itume wapelelezi wake humu nchini ili iwashike watu wanaotaka kurejesha taifa hili katika enzi ya 2007,” akaongeza.

Awali, wabunge saba wa ODM, wakiongozwa na John Mbadi (Suba Kusini) waliekeza kidole cha lawama kwa Ruto wakimtaja kama kiongozi mpenda fujo na anayepasa kudhibitiwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Wakiongea katika majengo ya bunge, wabunge hao walidai kuwa Naibu Rais na wafuasi wake ndio walichochea fujo hizo “kwa lengo la kutoa taswira kuwa analengwa na serikali kutokana na azma yake ya kuingia Ikulu 2022.”

“Dkt Ruto ni mtu ambaye anataka kutumia fujo ili kutimiza lengo lake la kuingia Ikulu 2022. Mtu kama huyo anafaa kuzuia mapema ili asisambaratishe nchini alivyofanya katika miaka ya nyuma,” akasema Bw Mbadi. Kauli hiyo iliungwa mkono na kiranja wa wengi Junet Mohamed.

Wakati huo huo, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro amedinda kujiwasilishwa kwa afisi za Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Nyeri, alivyoagizwa na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai.

Akiongea kwenye mahojiano katika runinga moja ya humu nchini Jumatatu, Bw Nyoro alisema hakufahamisha rasmi kuhusu agizo hilo akisema alipata habari hizo kupitia mitandao ya kijamii.

Mnamo Jumapili jioni Bw Mutyambai aliamuru kwamba Bw Nyoro na mwenzake wa Kandara Alice Wahome wasakwe na wahojiwe kuhusiana na fujo zilizotokea Murang’a wakati wa ziara ya Dkt Ruto.