Habari Mseto

Wandani wa Ruto wataka Kinoti afutwe kazi

December 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na ONYANGO K’ONYANGO

BAADHI ya viongozi wa Bonde la Ufa sasa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta amfute kazi Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), George Kinoti, kwa kujaribu kufufua kesi za ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008.

Ingawa DCI ilikuwa imesema haitafungua upya faili za kesi hizo ambazo uchunguzi wao ulishakamilika, viongozi hao walimshutumu Bw Kinoti kwa kujarabu kutonesha makovu licha ya jamii zilizohusika kukumbatia amani.

Magavana Jackson Mandago (Uasin Gishu) na Stephen Sang’ (Nandi) walimtaka Rais amfute kazi Bw Kinoti kama kweli hakuwa na habari kuhusu hatua ya kuwaagiza waathiriwa wa ghasia hizo kuandikisha upya taarifa zao katika makao makuu ya idara hiyo.

Bw Sang’ alimtaka Bw Kinoti kuwaomba Wakenya msamaha la sivyo ajiondoe kabla ya uchaguzi wa 2022.

“Hatuwezi kuwaruhusu baadhi ya watu wachochee watu wetu. Kwa hivyo Rais anafaa kumtimua Kinoti mara moja kwa sababu amedhihirisha wazi nia yake ya kuzamisha taifa hili kwenye ghasia tena,” akasema Bw Sang’ akihutubu katika kijiji cha Chepkemel, eneobunge la Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu.

“Kama viongozi, hatutakubali kesi hizo zifunguliwe upya ilhali jamii zimeridhiana,” akaongeza.Kwa upande wake, Bw Mandago alidai kuna mpango wa kuwatumia watumishi wa umma kuvuruga amani nchini lakini akaapa kuwa hawataruhusu hilo lifanyike.

“Hatutakubali kurejeshwa nyuma kuhusu suala hilo. Sisi ni viongozi ambao huhubiri amani na kuidumisha. Kwa sasa hatutaki masuala ya nyuma yatumike kuvuruga amani kati ya jamii zetu,” akasema Bw Mandago.

“Nimezungumza na wazee na wameniambia hawajasikia jambo lolote ambalo linatishia amani eneo hili,” akaongeza.