Habari Mseto

Wanne wakamatwa kwa kulaghai raia wa kigeni Sh29 milioni wakidai wangemuuzia dhahabu

September 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA wa upelelezi wa jinai Jumamosi wamesema wamewakamata washukiwa wanne katika eneo la Kasarani, Nairobi kwa kosa la kupokea pesa kwa njia ya ulaghai.

Washukiwa hao wanadaiwa kupokoea Sh29 milioni kutoka kwa mwanamume mmoja, raia wa kigeni, wakidai wangemuuzia dhahabu.

“Katika siku mbalimbali kuanzia Aprili 1, 2019, hadi Februari 28, 2020, wanne wao walimwambia mtu huyo ambaye ni raia wa kigeni – wakijifanya kuwa maafisa wa DCI – walitaka kumuuzia dhahabu kwa niaba ya afisa wa cheo cha juu katika DCI,” imesema taarifa ya DCI kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter.

Kulingana na DCI, washukiwa hao waliendelea kuitisha pesa kutoka kwa raia huyo wa kigeni hadi wakati ambapo walikamatwa. Washukiwa hao ni; Eric Otieno, Antony Achieng, George Kinuthia Mbugua na Arthur Caleb Otieno.

Wote wanne wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kasarani, na watafikishwa mahakamani Jumatatu kufunguliwa mashtaka kadhaa, ikiwemo kupokea fedha kwa njia ya ulaghai.