Wanne washtakiwa kosa la wizi wa Sh52 milioni kutoka KCB Thika
Na LAWRENCE ONGARO
MAHAKAMA ya Thika imepanga kusikiza kesi ya wizi wa pesa za benki ya Kenya Commercial Bank, Thika kwa siku tatu mfululizo, mashahidi wakiwa ni 30.
Washukiwa wanne waliofikishwa mahakamani Jumatano kwa wizi huo wa Sh 52 milioni ni ndugu wawili Halford Munene Murakaru, 32, na Charles Mwangi Murakaru, 30.
Wengine walioshtakiwa pamoja na washukiwa hao ni Julius Ndung’u na Shem Karimi, 32.
Washukiwa wa kwanza na wa pili walitetewa na wakili wao Bw Jack Oronga.
Wengine wawili waliwakilishwa na wakili Bi Waithera Mwangi.
Kesi hiyo ilisikizwa na hakimu mkuu wa Thika Bw Julius Mang’ea ambaye alimwagiza kiongozi wa mashtaka Bi Maundu kufanya hima kuwakabithi mawakili hao wawili stakabadhi zote wanazohitaji ili kuendelea na kesi kwa njia taratibu kabisa.
Hata hivyo, kesi hiyo itasikizwa rasmi Julai 15, 17, na 18 huku mashahidi wapatao 30 wakiorodheshwa kusimama kizimbani kutoa ushahidi wao.
Baadhi ya stakabadhi muhimu walizohitaji mawakili hao ni maelezo kamili kuhusu shtaka hilo, vyeti vya kuwatambulisha washukiwa hao, na stakabadhi kamili kutoka kwa benki ya Kenya Commercial Bank za kuonyesha kiasi cha fedha zilizoibwa, na alama za vidole kutoka kwa wataalamu wa maabara.
Washtakiwa walipofikishwa kizimbani walionekana wakiwa na wasiwasi huku wakificha nyuso zao wasitambulike na waliofika mahakamani.
Mahakama hiyo ilijaa pomoni huku kila mwananchi akitaka kuwaona washukiwa hao ambao waligonga vyombo vya habari mara ya kwanza walipofikishwa mahakamani mwaka 2017.
Wanne hao walioachiliwa kwa dhamana ya Sh 4 milioni, na izingatiwe walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani mnamo Novemba 17 na 18 mwaka wa 2017.
Ilidaiwa kuwa washukiwa hao walitumia ujanja mwingi kuingia katika hazina kuu ya benki ya Kenya Commercial Bank, iliyoko mjini Thika ambapo walidaiwa kuchimba shimo lenye urefu wa mita 30 kutoka nje ya benki hiyo huku likiwa na kina cha futi 10 kabla ya kufikia hazina ya pesa kwenye benki hiyo.
Ilidaiwa mpango huo wa kuchimba shimo hilo ulichukua muda wa miezi kadha kabla ya kukamilisha shughuli hiyo ya wizi.