Wanne wauawa wakazi wa Ikolomani wakipinga kampuni ya kuchimba dhahabu
WATU wanne wameuawa huku wengine sita wakijeruhiwa baada ya polisi kukabiliana na wachimbaji wadogo wa madini waliokuwa wakifanya maandamano dhidi ya kampuni ya uchimbaji madini katika Soko la Isulu, Kaunti ya Kakamega, Alhamisi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Magharibi, Issa Mahmoud, miongoni mwa waliojeruhiwa ni maafisa wawili wa polisi.
Wachimbaji hao walikuwa wakipinga hatua ya serikali kupatia kampuni ya Shanta Gold Limited leseni ya kufanya shughuli za uchimbaji katika maeneo ya Ikolomani. Walilalamikia kufurushwa katika maeneo tajiri kwa dhahabu ili kupisha mwekezaji huyo mpya kuchimba madini hayo ya thamani.
Katika makabiliano hayo, watu watatu walipigwa risasi na polisi, huku wanahabari kadhaa akiwemo mwanahabari wa NTV William Maina, wakijeruhiwa.
Vifaa vyao vya kazi na simu za mkononi viliharibiwa au kuibwa baada ya kuvamiwa na wachimbaji walioonekana kuwa na mori.
Mkutano wa kuwashirikisha wananchi kati ya wakazi, polisi, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA), Wizara ya Madini na mwekezaji wa uchimbaji dhahabu ulikatizwa ghafla na kundi la vijana.
Vijana hao waliokuwa wamejihami kwa marungu walikuwa wameletwa kwa magari manne aina ya Nissan matatu. Walivamia mkutano huo na kuwapiga waliokuwa wakiudhuria huku wakazi wakitawanyika kuokoa maisha yao