Wapokomo na Waorma kuungana kisiasa
NA MWANDISHI WETU
WAZEE wa jamii ya Kipokomo wamependekeza ushirikiano na wenzao wa jamii ya Waorma kwa nia ya kuleta uwiano na kuunda muungano, huku joto la kisiasa likianza kushuhudiwa katika kaunti ya Tana River.
Mkutano uliondaliwa na wazee wa Kipokomo katika kijiji cha Malindi ya Ngwena Jumamosi unakisiwa kujadili muungano na umoja kati ya jamii hizo mbili, kwa madhumuni ya jamii hizo mbili kupiga kura kwa sauti moja.
Katika mahojiano na Taifa Leo, mmoja wa viongozi ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa jamii hizo bili zilikuwa zikiwazia muungano wa viongozi kutoka jamii hizo mbili, watakao ongoza harakati za maendeleo.
“Tumefika mahali ambapo lazima yaliyopita yawe ndwele na tutazame maisha ya mbele na haswa uwezo wetu kiuchumi kama jamii, na tulete mezani kitakachowafaidi watu wetu, “alisema.
Na Stephen Oduor
Kigogo huyo alisema kuwa tayari baadhi ya viongozi kutoka jamii zote mbili walikuwa wamekwisha onyesha imani kwa wazo hilo, jambo ambalo limeashiria ukomavu wa viongozi hao kisiasa.
Ilibainika kuwa huu haukuwa mkutano wa kwanza bali wa pili ambapo wazee wa jamii hizo mbili wamekaa kulivakia njuga swala hilo, huku mkutano wa kwanza ukiwa katika kijiji cha Wayu, ambapo wazee wa jamii ya Waorma waliwapa wenzao wa Pokomo mapendekezo yao kulingana na mipangiluo hiyo .
Jamii ya Wapokomo wanatazamia kumrudisha Gavana Dhadho Godhana kumaliza hatamu ya pili, huku akisaidiwa na naibu kutoka jamii ya walio wachache, Seneta na Spika kutoka jamii ya Waorma, huku Wapokomo wakipewa nafasi ya mwakikishi wa akina mama.
Jamii ya Waorma kwa upande wao wanadai nafasi ya kuwa na gavana, huku wakiwa na viongozi wawili pinzani akiwemo aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo Hussein Dado na mbunge wa Bura Ali Wario Faya.
Iwapo jamii hizo mbili zitafanikisha mazungumzo na kukubaliana, basi muungano huo utaingia ugani kupambana na muungano wa aliyekuwa spika wa bunge la kaunti Dkt Abdi Nuh, ambaye anatarajiwa kupata kura za wapokomo wa maeneo ya Tana Delta katika muungano wake na kigogo wa siasa za kanda ya Pwani Bw Danson Mungatana.
Mwanasiasa huyo anapanga kuwania useneta katika muungano huo ambao umeivuta jamii za walio wachache, haswa jamii ya Wailwana.
Uwezekano wa kuwepo kwa muungano huo umekuwa ukibainika kwa wazi, huku mwakilishi bunge wa akina mama Bi Rehema Hassan na naibu wa gavana Bw Salim Batuyu wakionekana kuhusiana kwa karibu na Dkt Nuh kiasi cha kumwalika katika sherehe za kitamaduni.
Hata hivyo baadhi ya watu wamedai kuwa hakuwezi kuwa na muungano kati ya Wapokomo na Waorma, huku wakizitaja tofauti zao kama donda ndugu lisoweza sahaulika hata kwa sekunde moja.
Kwengineko, wachanganuzi wa kisiasa katika kaunti wamedai kuwa jamii ya Waorma kihistoria haiwezi mpigia debe mtu mwengine iwapo mtu wa jamii yao atakuwa amesimama kuwania kiti cha ugavana .
Hata hivyo Gavana Dhadho Godhana ameonyesha nia ya kufanikisha umoja kati ya jamii hizo mbili, huku akiwekeza mamilioni ya pesa katika ujenzi wa raslimali katika maeneo ya wafugaji hao, mojawapo ikiwa na ujenzi wa makao makuu ya kaunti, na hata hospitali kuu.
Gavana huyo pua amehusika katika kufungua miradi kadhaa ya maji katika maeneo hayo kame, mbaki na kuwanunulia wafugaji vifaa vya ukulima huku akiwahimiza kujaribu ukulima,jambo ambalo limewavutia viongozi kadhaa wa eneo hilo.