Wasafiri wakwama vituoni baada ya uchumi kufunguliwa
Na WAANDISHI WETU
MAMIA ya wasafiri waliotaka kuelekea katika kaunti ambazo zilifunguliwa jana baada ya kufungwa kwa miezi mitatu, walikwama vituoni katika maeneo tofauti ya nchi.
Uchunguzi wa Taifa Leo katika vituo mbalimbali Mombasa, Nairobi na magharibi ya nchi ulibainisha wasafiri wengi walikuwa na hamu ya kuelekea kwingine lakini hawakufua dafu.
Wamiliki wa magari ya uchukuzi hasa yanayoelekea Nairobi walisema hawako tayari kuanzisha shughuli zao kwa sasa kwani hawajapata vibali vipya vinavyohitajika hasa vyeti vya Covid-19 kutoka kwa Wizara ya Afya.
Meneja Mkurugenzi wa kampuni ya mabasi ya Coast Bus, Bw Ajaz Mirza alisema kuwa tayari wameanza kujipanga kurejelea biashara zao.
“Tunafurahia kufunguliwa kwa kaunti hizo na tutafuata sheria zote kuhakikisha kuwa wateja wetu hawaambukizwi virusi vya corona,” akasema Bw Mirza.
Naye, msimamizi wa kampuni ya mabasi ya Chania Genesis ofisi ya Mombasa, Bw Charles Gachuru alisema wanasubiri kuelezwa ni nini wanachohitajika kufanya kisha waanze biashara zao.
Bw Gachuru alisema kuwa kuendelea kwa kafyu kutawalazimu kubadilisha saa za gari kuondoka kutoka eneo moja hadi lingine.
Katika maeneo ya Pwani, wamiliki wa matatu zinazohudumu kati ya Kaunti za Mombasa na Kwale hatimaye walirejea barabarani hapo jana. Hata hivyo, wengi waliohojiwa walisema kanuni ya kubeba abiria nusu bado ni hasara kwao.
“Abiria akiwa amevaa maski na amesafisha mikono kabla ya kuingia ndani ya gari, hatuoni haja ya kupunguza idadi ya abiria,” akasema Bw Fadhili Amri makanga anayehudumu katika barabara kuu ya Mombasa Lunga Lunga.
Na katika Kaunti ya Siaya, mmoja wa wahudumu wa mabasi yanayoelekea Nairobi alisema magari yao mengi yalikuwa yameng’olewa viti ili yasafirishe mizigo, na watahitaji kuyafanyia ukarabati kwanza. Kwingineko, Gavana wa Nakuru, Bw Lee Kinyanjui alikosoa uamuzi wa Rais Uhuru Kenyatta kuondoa marufuku ya kusafiri katika kaunti za Nairobi na Mombasa.
Bw Kinyanjui alisema jana kuwa huenda maambukizi ya virusi vya corona yakaongezeka zaidi katika kaunti ambazo zimerekodi visa vichache.
Ripoti za Phyllis Musasia, Diana Mutheu, Mishi Gongo na Dickens Wasonga
Kwenye taarifa yake, alisema tayari watu wengi wameonyesha kuzembea katika kufuata kanuni zilizotolewa na idara ya afya ili kujikinga na maambukizi.
“Virusi vya corona haviwezi kusafiri vyenyewe ila hutokea kufuatia kutangamana na watu wengi haswa safarini. Safari za kutoka eneo moja hadi lingine zitachangia sana kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19,” akasema.
Kulingana naye, huenda siku za hivi karibuni Kenya ikalemewa na maambukizi na kukosa kudhibiti idadi kubwa ya wagonjwa iwapo watu watazidi kupuuza kanuni zinzofaa.