Wasamburu waipa serikali siku 2 wamwachilie Lesiyampe
Na KNA
VIONGOZI wa jamii ya Samburu wameipa serikali muda wa siku mbili kuyaondoa mashtaka yanayomkabili katibu katika wizara ya Kilimo Richard Lesiyampe wakitaja vita dhidi ya ufisadi kama vilivyoingizwa siasa.
Wabunge Alois Lentoimaga (Samburu Kaskazini), Naisula Lesuuda (Samburu ya Kati ) na Mwakilishi wa kike wa kaunti hiyo Maison Leshoomo walisema kwamba ingawa wanaunga mkono vita dhidi ya ufisadi, mashtaka dhidi ya Bw Lesiyampe hayana mashiko kwa kuwa hakuhusika wala kugusa pesa za kununua mahindi.
Bw Lesiyampe na wengine wanane wanakabiliwa na mashtaka kuhusiana na sakata ya Sh 6 bilioni za kununua mahindi katika Bodi ya Kitaifa ya nafaka na mazao (NCPB).
“Bw Lesiyampe hagusi pesa zinazotoka katika hazina kuu ya kitaifa. Ni serikali iliyoagiza ununuzi wa mahindi wakati wa kiangazi, Kwa nini katibu huyo analaumiwa?,” akasema Bw Lentoimaga jana katika kambi ya ngamia ya Yale mjini Maralal mbele ya Naibu Rais William Ruto.
Mbunge huyo alimtaka Bw Ruto na Rais Uhuru Kenyatta waingilie kati ili kusisitisha mashataka yanayomkabili katibu huyo ambaye anatoka eneo hilo.
“Tunataka mashtaka yote yatupiliwe mbali. Rais Kenyatta ana uwezo wa kisheria kufanya hivyo,” akadai Bw Lentoimaga.
Kauli yake iliungwa mkono na Bi Leesuda na Bi Lesuuda ambao walisema kwamba uchunguzi wa kamati ya bunge kuhusu kilimo kivyovyote haikumpata Bw Lesiyampe na hatia.
Kwa upande wake Gavana Moses Lonolkulal aliwaunga wabunge hao na kusema kwamba taaluma za watu muhimu nchini kama Bw Lesiyampe huenda ikaharibiwa kutokana na madai ya uongo.