Washangaza kung'ang'ania vyuma kuukuu baada ya ajali
Na GEOFFREY ONDIEKI
Kioja kilizuka eneo la Kaptembwa mjini Nakuru baada ya wakazi kung’ang’ania vyuma kuukuu wakati lori la kusafirisha vyuma hivyo lilipopoteza mwelekeo na kuanguka karibu na mzunguko wa Eveready.
Kulingana na walioshuhudia ajali hiyo, lori hilo lilikuwa linaendeshwa kwa kasi mno. Dereva wa lori alishindwa kulidhibiti kwenye kona na kupoteza mwelekeo na hivyo kuanguka.
Hata hivyo dereva huyo alinusurika japo alipata majeraha madogo. Wakazi walipata fursa na kuvuna kwa kuokota vyuma vilivyotapakaa barabarani. Ni hatua ambayo iliwaacha wengi vinywa wazi ikizingatiwa kuwa wakazi wanajaribu kuokota vyuma ambavyo kwa msingi si vya dhamani.
Mmiliki wa lori alipofika ndipo wakazi walitawanyika na magunia yaliyokuwa yamejaa vyuma kuu kuu.
Hata hivyo alikataa kuzungumza na wanahabari kwa kile kilichoonekana kuwa alikuwa amekerwa na hatua ya wakazi kupora vyuma.
Tabia ya wakazi kung’ang’ania mali wakati ajali inapofanyika si geni humu nchini haswa mjini Nakuru. Wiki mbili zilizopita wakazi walijaribu kung’ang’ania lori la mafuta ya petroli lililokuwa linavuja.
Hata hivyo polisi walikuawa macho na kufunga barabara hiyo na kuzuia wakazi kukaribia mahali hapo.