Habari Mseto

Washukiwa wa mauaji kuzuiliwa siku 12

August 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Kibera Jumanne iliamuru mfanyabiashara Chris Philip Obure na mlinzi wake Robert John Ouko Bodo wazuiliwe kwa siku 12 kuhojiwa kuhusiana na mauaji Kelvin Omwenga, yaliyotokea Jumamosi iliyopita katika mtaa wa Kilimani, Nairobi.

Hakimu mwandamizi Bw Derrick Kuto alisema polisi wanahitaji muda wa kutosha kuwahoji, hata baada ya mawakili Prof PLO Lumumba na Otieno Arum kupinga ombi hilo.

Bw Kuto aliagiza washukiwa hao warudishwe tena kortini Septemba 4, 2020, polisi waeleze ikiwa wamekamilisha uchunguzi na kuwafungulia shtaka wanaume hao wawili.

Mahakama ilisema Bw Obure amekiri bastola iliyotumika kuua ni yake na ilichukuliwa na Bw Ouko bila idhini yake.

Ombi la kuzuiliwa kwa wawili hao liliwasilishwa na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ODPP) kupitia kwa Bw Allan Mogere.

Bw Mogere aliomba wawili hao wazuiliwe kwa siku 14 kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi wa kesi ya mauaji watakayoshtakiwa.

Omwenga aliyekuwa na umri wa miaka 28 alipigwa risasi akiwa katika makazi yake kwenye jengo la Galana Suites, Kilimani usiku wa Agosti 22, 2020.