• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:31 PM
Washukiwa wa MRC wazuiliwa kwa siku 14

Washukiwa wa MRC wazuiliwa kwa siku 14

Na FADHILI FREDRICK

MAHAKAMA mjini Kwale imewazuia washukiwa 17 wanaodaiwa kuwa wanachama wa kundi la Mombasa Republican Council (MRC) kwa siku 14 ili kuwapa polisi nafasi ya kufanya na kuwasilisha ripoti ya uchunguzi.

Washukiwa hao wakiwa wengi ni wazee wa kati ya umri wa miaka 41 hadi 81 walikabiliwa na mashtaka ya kukusanyika na kufanya mkutano bila idhini ya polisi kinyume na kifungu cha 5(2) cha sheria za Kenya.

Vile vile washukiwa walishtakiwa kwa nia ya kuzua vurugu kinyume na kifungu cha 96(c) cha kanuni za ya adhabu.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mnamo Aprili 2, wanachama hao walikuwa na karatasi ambazo zilikuwa na maneno yaliyoandikwa “Pwani Si Kenya” ikiashiria kwamba wanaweza kuvunja sheria za nchi.

Lakini wakiwa mbele ya Hakimu Mkazi Patrick Wambugu, washukiwa hao mmoja baada ya mwingine walikanusha mashtaka hayo, huku wakiwalaumu polisi kwa kuwanyanyasa.

Upande wa mashtaka uliomba korti kutowapa washukiwa hao dhamana ukisema tu punde washukiwa hao walipokamatwa eneo la Kibundani huko Diani jioni yake maafisa wa polisi walivamiwa.

“Tunashuku kuvamiwa kwa polisi waliokuwa wakishika doria kunahusiana na kukamatwa kwa washukiwa na hivyo tunaomba mahakama kuwazuilia washukiwa,” ukasema upande wa mashtaka.

Hata hivyo, mshukiwa mmoja alijitetea na kusema kwamba hawana uhusiano wowote na waliovamia polisi.

“Tunataka wale ambao walishambulia polisi waletwe mahakamani na watuambie kama walishambulia maafisa wa polisi kwa niaba yetu,” akaomba.

Na washukiwa wawili, Bw Hamisi Mohammed na Said Hassan waliililia mahakama kuwaachilia kwa dhamana kwani afya yao ni duni.

“Hivi karibuni nilikuwa mjini Tanga kufanyiwa operesheni na afya haija kuwa sawa kwa hivyo naomba mahakama iniachilie kwa dhamana,” akasema.

Washukiwa wengine ni Salim Nassir, Kassim Masudi, Juma Samini, Hamad Said, Ali Said, Abdallah Said na Abdallah Ali.

Na wengine ni Hassan Bakari, Ali Ali, Kassim Hassan, Hemed Abdallah, Kassim Said, Omari Hamisi, Mbwana Ali, na Abdallah Haji.

Washukiwa hao watafikishwa tena mahakamani Aprili 18.

You can share this post!

Maafisa watakiwa kuomba wakazi msamaha

Wanahabari wakataa tuzo za Wizara ya Kawi

adminleo