Washukiwa wa ufisadi kuzimwa kuingia nchini Uingereza
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI ya Uingereza inapanga kuwanyima ruhusa ya kuingia nchini humo Wakenya wanaohusishwa na ufisadi, balozi wa Uingereza nchini anayeondoka Nic Hailey amesema.
Bw Hailey alieleza kuwa taifa lake pia halitawaruhusu watu kama hao kuendesha shughuli zozote nchini Uingereza.
“Watu kama hao hawataruhusiwa kuingia Uingereza kwani watanyimwa visa. Kwa hivyo, tunaitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kutupa orodha ya watuhumiwa wa ufisadi ili tuwazime kuingia Uingereza,” akasema Hailey Jumatano jioni.
Alisema hayo alipomtembelea Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Twalib Mubarak afisini mwaka katika Jumba la Integrity Centre, Nairobi.
Bw Hailey pia alisema wale ambao wameshtakiwa kwa makosa ya ufisadi wanapaswa kujiuzulu nyadhifa za serikalii ili kutoa nafasi kwa uchunguzi huru kuendeshwa dhidi yao.
“Maafisa kama hawa wanafaa kujiondoa afisini kwa muda kwa sababu wanaweza kutumia ushawishi wao kuhujumu uchunguzi ilivyo sasa ambapo wangali afisini,” akasema.
Kujisaidia
Balozi huyo alisema Uingereza imejitolea kuisaidia Kenya katika vita dhidi ya ufisadi huku akiitaja uovu huo kama kansa kuu inayoathiri uchumi wa taifa hili.
Bw Hailey alifichua kuwa amekuwa akifanya mashauriano ya kila mara na EACC na ana habari kwamba hivi karibuni maafisa fulani wa hadhi ya juu serikalini watakamatwa kwa makosa hayo.
Alikubalia kuwa kesi za ufisadi huchukua muda mrefu kukamilishwa na hivyo mchakato huo unahitaji maandalizi kambambe haswa katika zoezi la ukusanyaji ushahidi.
“Hii ndio maana tumejitolea kusaidia Kenya katika vita dhidi ya uovu huu,” Bw Hailey akasema huku akiongeza kuwa Uingereza itahimiza kukomeshwa kwa msururu wa mikutano kuhusu jinsi ya kupambana na ufisadi.
“Vilevile, Uingereza itashirikiana na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) katika mpango wa kuhakikisha kuwa kesi za ufisadi zinakuwa thabiti,” akasema.
Kwa upande wake, Bw Mbarak alisema maafisa wa tume yake watakuwa wakitembelea Uingereza kila mara kusaka usaidizi kuhusiana na kesi za ufisadi.