Habari Mseto

Wasiwasi jeshi kutoka Somalia likitua kwenye mpaka wa Kenya

December 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MANASE OTSIALO

HALI ya wasiwasi imezuka katika kaunti ya mpakani ya Mandera baada ya Somalia jana Jumanne kuwatuma wanajeshi wake karibu na mpaka wa Kenya, saa chache tu baada ya Kenya na nchi hiyo kukatiza rasmi uhusiano wao wa kibalozi.

Wenyeji waliambia Taifa Leo kuwa waliwaona wanajeshi kutoka Somalia wakishika doria mpakani kama njia ya kuthibitisha kukatizwa kwa uhusiano huo.

“Tumeamka na kuwapata wanajeshi wa Somalia wakishika doria mpakani. Hali hii haijawahi kuonekana na imetushangaza sana,” akasema mkazi mmoja aliyejitambulisha kama Ali Abdille.

Magari ya kivita na wanajeshi hao yalikuwa katika maeneo tofauti ya mpakani, hali hiyo ikiwafanyabaadhi ya wakazi kuanza kuhama makwao wakihofia kuzuka kwa mapigano kati ya wanajeshi wa Somalia na Kenya.

Mmoja wa afisa wa kijeshi wa ngazi ya juu katika Kaunti ya Mandera alithibitisha kufika kwa wanajeshi hao kutoka Somalia maeneo ya mpakani.

“Tuna habari kuhusu yale yanayoendelea mpakani, lakini hilo ni suala ambalo litaamuliwa na viongozi wetu wakuu kule Nairobi,” akasema mwanajeshi ambaye hakutaka anukuliwe.

Tukio hilo limefuatia na hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kumwalika hapa Kenya Rais Muse Bihi wa Somaliland, ambayo imejitenga kutoka kwa Somalia.

Muda mfupi baada ya kikao cha Rais Kenyatta na Rais Bihi mnamo Jumatatu, Waziri wa Habari wa Somalia, Osman Dubbe alitangaza kuwa nchi hiyo imekatiza uhusiano wake na Kenya.

Bw Dubee alisema Kenya imekuwa ikiingilia masuala ya ndani ya Somalia na kuvuruga uhuru wa nchi hiyo kujitawala.

“Tunaomba serikali yetu na ile ya Somalia wamalize uhasama huu ili kuwe na amani kati ya nchi hizo mbili,” akasema Isaack Adan, mfanyabiashara mjini Mandera.

Wakazi wa mji wa Mandera hutegemea bidhaa kutoka Somalia ikizingatiwa kwamba Nairobi iko mbali sana na mji huo wa Kaskazini Mashariki.

“Hali hii itaathiri maisha yetu ya kawaida kibiashara kati ya Mandera na Somalia. Huwa tunaaagiza bidhaa nyingi kutoka Mogadishu kuliko Nairobi,” akaongeza.