Habari Mseto

Wasiwasi ugonjwa wa macho mekundu ukizuka Busia

May 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA SHABAN MAKOKHA

WASIWASI umewakumba wakazi wa Kaunti ya Busia baada ya mkurupuko wa ugonjwa wa macho, usiojulikana, katika kaunti ndogo saba kuripotiwa.

Serikali ya kaunti hiyo inasema imenakili visa 180 vya ugonjwa huo wa kugeuza macho kuwa mekundu kupita kiasi (conjunctivitis) miongoni mwa wanafunzi na wakazi.

Daktari wa macho katika Kaunti, Harriet Kavere, alisema baadhi ya maeneo ambako ugonjwa huo uligunduliwa juzi ni pamoja na Matayos, Nambale na Funyula.

“Tumeingiwa na wasiwasi kwamba ugonjwa huu wa macho unaenea kwa kasi na katika hali ya kutisha,” akasema Dkt Kavere.

Wekundu wa macho kwa waathiriwa hutokea baada ya virusi na bakteria kusababisha mwasho kwenye kope za macho. Daktari huyo alisema ugonjwa huo unasababishwa na virusi vinavyojulikana kama “Adenoviruses” ambavyo pia husababisha magonjwa mengi kama vile, ugonjwa wa mapafu, kutapika, miongoni mwa mengine.

Alisema kando na wekundu wa macho, dalili nyingine za ugonjwa huo ni kuvimba kwa macho na kutokwa na majimaji ya manjano.

“Ugonjwa huu husambaa kwa haraka. Mtagusano na wagonjwa au kutumia vitu kadha na wao pia ni njia nyingine ambazo ugonjwa huu husambaa,” akaeleza.

Ugonjwa huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza katika kaunti ndogo za Teso Kaskazini na Teso Kusini kabla ya kuenea kwa kasi katika maeneo mengine.

Idara ya afya katika Kaunti ya Busia imetoa wito kwa wakazi kuchukua hatua za tahadhari za kudumisha usafi kama vile kunawa mikono kila mara.

“Kile kilianza kama mwasho mdogo kwenye jicho langu la kushoto sasa umeenea katika jicho la kulia na kuathiri watu wote katika familia yangu,” akasema Bw Patrick Okelo, ambaye ni mkazi.

Wagonjwa wameshauriwa kutumia karatasi shashi wanapopangusa macho yao na wakome kutumia kwa pamoja vitu kama vile taulo, mto au vipodozi vya macho.

Dkt Kavere alitoa wito kwa mtu yeyote ambaye anaweza kupatwa na dalili za ugonjwa huo kama vile macho kugeuka kuwa mekundu, mwasho na kutoweza kuona vizuri kusaka matibabu haraka.

“Aidha, tunatoa wito kwa raia kuwa watulivu, wazingatie masharti ya kuzuia maambukizi na watoe ripoti kuhusu visa vya maambukizi kwa asasi husika za serikali,” akaeleza.