Wasiwasi visa vya wanaouliwa na radi vikiongezeka
HUZUNI na hofu imetanda Kaunti Ndogo ya Mumias Mashariki baada ya watu watatu kuuawa na radi ambayo imeacha watu wengi wakiwa na majeraha katika muda wa wiki moja.
Tukio la hivi punde lilihusisha kifo cha wanawake wawili waliopigwa na radi iliyopiga nyumba waliyokuwa katika kijiji cha Elukoto huko Isongo.
Watu wengine wawili wanauguza majeraha mabaya kutokana na tukio hilo.
Kisa hicho kilitokea nyumbani kwa Nicholas Omamo Walunya mvua ilipokuwa ikinyesha katika eneo hilo Jumamosi jioni, Juni 29, 2024.
Wakazi walisema wamekuwa wakishuhudia wimbi kubwa la radi ambayo imekuwa ikipiga eneo hilo bila kusababisha uharibifu kwa miaka mingi.
Siku ya maafa, Bw Walunya alikuwa ndani ya nyumba pamoja na mkewe Demtila Osimbo na wageni wawili waliowatembelea kujisitiri mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha eneo hilo.
“Tulipokuwa tukizungumza katika nyumba mwendo wa saa kumi na moja jioni, radi kali ya kutisha ilipiga na kumpiga mke wangu, Demtila, 57, na mmoja wa wageni aliyejulikana kama Rose Chimila kutoka Shikomari huko Navakholo na kuwaua papo hapo. Ndugu yangu na mtoto wake mmoja ambao pia walikuwa nyumbani kwangu walijeruhiwa,” akasema Bw Walunya.
Majeruhi, David Omamo na Difina Mukoya walikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Makunga na hospitali ya St Mary’s Mumias mtawalia ambapo wanaendelea kupata nafuu.
Tukio hilo lilitokea siku ambayo mwathiriwa mwingine Rashid Andewa (26) aliyepigwa na radi alikuwa akizikwa katika kijiji jirani cha Shianda.