Wasutwa kwa kupinga mageuzi sekta ya sukari
Na RUSHDIE OUDIA
WAKULIMA na wafanyakazi wa sekta ya miwa wamewakashifu wanasiasa kutoka eneo la Magharibi wanaopinga mageuzi katika sekta hiyo.
Miongoni mwa hatua ambazo serikali kuu imetangaza ni kupiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka nje ya nchi ili kuzuia sukari ya bei nafuu ambayo imeathiri wakulima wa humu nchini.
Wadau katika sekta ya sukari chini ya mwavuli wa chama cha kitaifa cha Mashirika ya wakulima wa miwa (KNASFO) walisifu kanuni za kudhibiti sukari za mwaka huu ikiwemo hatua ya serikali kukodisha viwanda vitano vya sukari kwa kampuni za kibinafsi.
Mwenyekiti wa KNASFO, Bw Saulo Busolo aliwashutumu wanasiasa kwa kuingilia juhudi za kufufua sekta ya sukari ambayo imeteseka kwa miaka mingi.
“Wanaojinufaisha kupitia siasa na wanafikiri kwamba wanaweza kuja na kujijenga kwa kutoa taarifa za kupotosha kuhusu sekta ya sukari,” alisema Bw Busolo.
Alisema wanasiasa wanaopinga mageuzi hayo wana lengo la kuvuruga sekta hiyo na kuiharibu kabisa. Hata hivyo, alimsifu Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya kwa kusimama imara kushinikiza mageuzi hayo kupitia ripoti ya jopokazi la kitaifa la sekta ya sukari.
Bw Busolo aliyezungumza akiwa Kisumu Jumanne, alisema hatua ya serikali itatatua masuala ya kisera katika sekta ya sukari.
Alisema marufuku ya kuingiza sukari nchini yatakahakikisha kuna soko tayari na kwa hivyo kuimarisha sekta hiyo na hata kuwa na ya kuuza nje ya nchi.
“Wakulima wa miwa wataweza kutoa tani 9.89 milioni za miwa huku mahitaji ya viwanda humu nchini ikiwa ni tani 1.09 milioni kwa mwaka,” alisema Busolo.
Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi wa mashamba ya miwa Bw Francis Wangara aliwataka wanasiasa wakome kuingilia sekta hiyo.