Wataalamu nao waunga mkono Katiba igeuzwe
Na KITAVI MUTUA
WATAALAMU wa masuala ya katiba wameunga mkono shinikizo za kuifanyia mageuzi Katiba ya sasa, wakisema kuwa kuna haja ya kutathmini baadhi ya vipengele vyake.
Shinikizo hizo zimekuwa zikiendeshwa na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga, akisisitiza hitaji la kuangazia baadhi ya mapengo yaliyopo.
Wakili maarufu wa kikatiba Nzamba Kitonga (pichani), alisema kuwa imefikia wakati ambapo katiba hiyo inapaswa kutathminiwa upya, ili kuangazia masuala ambayo tayari yamegunduliwa kuwa “tata” kwenye Katiba iliyopitishwa 2010.
Bw Kitonga, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu, iliyoandika Katiba hiyo, alisema kuwa kuna hitaji la utathmini wake, kwani baadhi ya Wakenya wanahisi kutengwa katika utaratibu wa uongozi wa nchi.
“Kama Kamati ya Wataalamu, tulitarajia kwamba utathmini mpya wa Katiba ungefanywa baada ya miaka saba hadi kumi, ili kuangazia mapengo ambayo yangekuwa tayari yamedhihirika katika utekelezaji wake,” akasema Bw Kitonga.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Kitonga alisema kwamba mpangilio wa sasa wa matawi makuu ya serikali unapaswa kuangaliwa upya, ili kuimarisha ushirikishi wa kisiasa na kikabila, kupunguza kiasi cha fedha kinachotumika kuziendesha na kuimarisha utendakazi wa Idara ya Mahakama.
Alieleza kuwa Katiba hiyo ni nzuri kwa ustawi wa Kenya, ila ina mapengo kadhaa ambayo lazima yashughulikiwe.
Hasa alikosoa mfumo wa urais, ambapo anayeshinda kinyang’ayiro cha urais hubuni serikali, akisema kuwa imedhihirika kwamba haiendelezi nchi, ila unazua miganyiko ya kikabila. Alisema kuwa mfumo huo unaziacha nje jamii nyingi katika utaratibu wa uongozi wan chi.
“Rasimu ambayo tulibuni ilijumuisha mifumo ya utawala ya urais na bunge, ili kuvipa nafasi vyama vya kisiasa na kupunguza taharuki na hali ya ushindani usiofaa katika siasa zetu,” akasema.
Alieleza kuwa Katiba iliyopo kwa sasa ilifanyiwa mageuzi na wanasiasa kwa kuingiza mfumo wa urais, ambao ulikuwa umekataliwa na Wakenya kwenye shughuli za mageuzi ya katiba.
“Tulikuwa tumebuni afisi ya Kiongozi wa Upizani, ambapo pia angekuwa akishiriki katika vikao vya Bunge. Hata hivyo, kipengele hicho kiliondolewa, hali ambayo imewafanya Wakenya wengi kutengwa katika mfumo wa utawala wa nchi,” akaeleza.
Alisema kuwa chini ya rasimu hiyo, Bw Odinga na mgombea-mweza wake,Kalonzo Musyoka ambao walishindwa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wangekuwa na afisi zao, ili kuwawezesha kufuatilia utendakazi wa serikali ya Jubilee.
Wakili Bobby Mkangi, ambaye pia alikuwa mwanakamati wa tume ya kubadilisha katiba, alisema kuwa hawakutarajia kwamba serikali ya kitaifa na zile za kaunti zingegeuzwa kuwa majukwaa ya ufujaji wa fedha za umma.
“Ni kweli kwamba baraza la mawaziri ni ndogo ikilinganishwa na awali, ila tungali tunatumia fedha nyingi kulipa mishahara ya maafisa katika serikali zote mbili,” akasema.