Habari Mseto

Wataalamu wabashiri kudorora kwa uchumi serikali ikiandaa bajeti ya Sh4.2 trilioni

June 12th, 2024 1 min read

NA BENSON MATHEKA

KUNA uwezekano mkubwa wa uchumi wa Kenya kudorora wa asilimia tano mwaka huu licha kukuza vyema mwaka jana.

Wataalamu, wakiwemo wa Benki ya Dunia wanasema hatua hii itachangiwa na masuala kadhaa ambayo serikali imepuuza au kujivuta kutatua kama mfumuko wa gharama ya maisha na kuanzishwa kwa aina nyingi za ushuru ambao ni mzigo kwa raia na wafanyabiashara na wawekezaji.

Kulingana na wataalamu wa Benki ya Dunia deni kubwa ambalo serikali inazidi kuongezea litafanya uchumi kudumaa japo Kenya itadumisha nafasi yake kuwa na uchumi bora Afrika Mashariki.

Wanaonya kuwa sera za serikali zitainyima mapato licha ya kubebesha raia mzigo wa ushuru.

Katika ripoti yake, Benki ya Dunia inasema japo Pato halisi la Taifa liliongezeka kwa asilimia 5.6 mwaka jana kutoka asilimia 4.9 mwaka wa 2022, litapungua mwaka huu hadi asilimia tano tu.

Shirika hilo la kimataifa linasema kwamba ukuaji wa mwaka jana, ulitokana na kufufuka kwa sekta ya kilimo kufuatia kuimarika kwa hali ya hewa na utalii ambao ulichukua mkondo wa ukuaji.

“Kufufuka kwa sekta muhimu ya kilimo kufuatia hali nzuri ya hewa kulichangia ukuaji wa uchumi 2023 huku utalii ukichangia hali bora ya uchumi mwaka huo,” inasema ripoti ya Benki ya Dunia.

Ripoti inasema kuwa Kenya imejikwaa kwa bidhaa inazouza nje ya nchi ambazo hazikuchangia pakubwa. “Kenya haijaongeza bidhaa zake katika miaka ya hivi majuzio na imepoteza ushindani wake katika masoko inayouza nje ya nchi,” inaeleza.

Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia inajiri wiki moja kabla ya serikali kuwasilisha bajeti yake Bungeni Alhamisi wiki hii.

Katika makadirio ya mwaka huu serikali imendaa bajeti ya Sh4.25 trilioni hadi Juni 30 2025 ikiwa imeongezeka kutoka Sh3.6 trilioni mwaka huu wa kifedha.

Onyo la wataalamu kuhusu kudorora kwa uchumi mwaka huu linajiri huku serikali ikikadiria kuwa Pato la Taifa litakua kwa asilimia 5.2 kati ya mwaka huu na 2026.