Habari Mseto

Wataalamu washutumu vyuo vikuu kwa kutoa mafunzo duni

September 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

KUONGEZEKA kwa idadi ya vijana wanaohitimu kutoka vyuo vikuu na kukosa au kushindwa kufanya kazi inayolingana na masomo yao kumefanya ubora wa elimu ya vyuo vikuu nchini kutiliwa shaka.

Wataalamu wa masuala ya uchumi na ajira wanasema vijana wengi wanaohitimu vyuo vikuu huwa hawajatayarishwa kikamilifu kufanya kazi.

“Waajiri hupendelea vijana wanaohitimu kutoka vyuo vya kiufundi kuliko wanaopata digrii. Tunafaa kuchunguza ubora wa digrii zinazotolewa na vyuo vikuu nchini,” asema Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri (FKE), Jackline Mugo anasema.

Kulingana na Shirika la Takwimu (KNBS), kuna vijana 6 milioni wasio na kazi nchini wakiwemo walio na shahada za digrii.

Watalaamu wa uchumi wanasema mbali na ubaguzi katika uajiri na uhaba wa nafasi za kazi, vyuo vikuu nchini haviwaandai wanafunzi vyema kwa maisha baada ya kuhitimu.

Kulingana na Bi Mugo, waajiri huwa wanatarajia wanaohitimu kuwa na ujuzi unaohitajika.“Inabidi waajiri kutumia pesa nyingi kuwafunza kazi wanaotoka vyuo vikuu kwa sababu huwa hawana ujuzi unaotakikana.

Hii inafanya waajiri wengi kuamua kuajiri wanaotoka vyuo vya kiufundi, ambao wana uwezo wa kufanya kazi bila mzigo mkubwa wa mafunzo,” asema Bi Mugo.

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha anasema baadhi ya vyuo vikuu vimetekeleza jukumu lake la kuandaa wanafunzi vyema vikilenga biashara.

“Baadhi ya wanafunzi huwa wanapata shahada zisizo na maana kabisa,” Profesa Magoha alisema alipowahutubia wakuu wa vyuo mapema mwaka huu.Anapendekeza vyuo vikuu vipunguzwe na viwe vikifunza kozi ambazo zinawaandaa wanafunzi vyema kwa kazi na sio tu kazi za ofisini.

Wataalamu wanasema mfumo wa elimu nchini unahitaji mabadiliko makubwa ikiwa Kenya inataka kukuza wataalamu wa sekta mbalimbali.Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Wandia Njoya anasema wakati umefika wa kuondoa shahada kama idhibati ya elimu ya juu.

“Tunahitaji kuwa na mfumo usiohusisha shahada, mbali unaokuza tajiriba na taaluma kuanzia viwango vya chini vya elimu,” asema Dkt Wandia.

Mbali na ubora wa masomo kutiliwa shaka, baadhi ya vyuo vikuu vimelaumiwa kwa kutoa kozi ambazo haziwafai wanafunzi, au ambazo hazijaidhinishwa na Baraza la Elimu ya Juu (CUE).

Hii inafanya vyama vya wataalamu katika sekta husika kukataa kuziidhinisha, na hivyo wanaohitimu kukosa vibali vya kuhudumu au kuajiriwa.

Wataalamu wanaonya kuwa idadi kubwa ya vijana waliosoma na hawana kazi ni janga la kijamii, kiuchumi na pia tishio kwa usalama.