Habari Mseto

Watahiniwa wa KCSE wakubali kuhamishwa

November 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

WATAHINIWA wa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) katika Kaunti ya Tana River kutoka Shule ya Upili ya Majengo, ambao wikendi walikataa kuhamishwa hadi shule ya sekondari ya Ndura hatimaye wamekubali kuhamishwa.

Wanafunzi hao walikuwa wamelalamika wakidai wanavurugwa kiakili kabla ya mtihani huo.

Kuhamishwa kwao kulichangiwa na mafuriko kwenye mto Tana kutokana na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa eneo hilo.

“Itatuchukua muda mwingi kufikisha mtihani baada ya kusafiri kilomita 35 kupitia boti ambayo inatumia lita 50 ya mafuta kila siku. Ingawa ilikuwa rahisi kwa KCPE kufanyika katika hali kama hiyo, KCSE huchukua muda mwingi,” akasema mwalimu aliyeunga mkono kuhamishwa kwa watahiniwa hao.

Wanafunzi hao 22 ambao ni wasichana sita na wavulana 16 baadaye walikubali kufanya mitihani katika shule ya Ndura, baada ya Mkurugenzi wa elimu Kaunti ndogo ya Tana River Abdi-Aziz Nuh kuingilia suala hilo.

“Tulifanikiwa kuwahamisha wanafunzi hao Jumamosi na kwa sasa wapo katika shule ya upili ya Ndura tayari kufanya mtihani huo. Tumegharimia kila kitu ikizingatiwa kwamba mto Tana unaendelea kufurika,” akasema Bw Nuh.

Mkurugenzi wa elimu ukanda wa Pwani Hassan Duale naye alisema kwamba mikakati yote ya usalama imewekwa ili kuzuia udanganyifu wakati wa mtihani huo.

“Tumeimarisha usalama na polisi watakuwa wakitoa ulinzi mkali katika vituo vyote vya kufanya KCSE. Tatizo pekee ni hali ya hewa isiyotabirika lakini tumejipanga kukabiliana na hali yoyote ile,” akasema Bw Duale.

Mtihani wa KCSE unaanza leo kwenye vituo 10,287 huku mvua ikiendelea kunya maeneo mengi nchini.

Wanafunzi 699,745 wanatarajiwa kufanya mtihani huo ikilinganishwa na 664,585 mwaka jana

Kama tu mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane(KCPE) uliotamatika Alhamisi wiki jana, KCSE inatarajiwa kufanywa chini ya ulinzi mkali na kufuatiliwa kwa makini na Baraza la Kitaifa la Mtihani (KNEC) hasa baada ya onyo kutolewa kwa watahiniwa wanaopanga kushiriki udanganyifu.

Serikali inatarajiwa kuwatuma maafisa wa usalama katika vituo mbalimbali vya kufanya mtihani huo ili kuzuia kisa kama kile cha mwaka jana ambapo matokeo ya wanafunzi 3, 427 kwenye vituo 44 kutoka kaunti 16 yalifutiliwa mbali. Mwaka wa 2017, watahiniwa 1,205 hawakupata matokeo yao baada ya kufutiliwa mbali kutokana na kushiriki udanganyifu.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Knec Dkt Mercy Karogo jana alisema wafanyakazi 70,790 watatumika kuendesha shughuli mbalimbali wakati wa mtihani huo.

Dkt Karogo alihakikishia taifa kwamba mipango na maandalizi yote ya mtihani huo yamekamilika.

“Hatuwezi kuruhusu taifa letu lirejee katika enzi za zamani ambapo wizi wa mitihani ulishamiri. Tangu mageuzi makubwa yatekelezwe na serikali 2016, kumekuwa na visa vichache vya udanganyifu,” akasema Dkt Karogo.