Habari Mseto

Wataka kilio cha wauguzi kisikilizwe kabla BBI

December 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

SHABAN MAKOKHA na DENNIS LUBANGA

SERIKALI imetakiwa kuzungumza na wahudumu wa afya wanaogoma ili kutatua mzozo huo ambao umelemaza huduma za afya nchini kwa wiki moja sasa.

Baadhi ya viongozi waliitaka serikali kusimamisha mchakato wa kubadilisha katiba ili kutatua mzozo unaokumba sekta ya afya.

Viongozi wa kidini na wanasiasa kutoka eneo la Magharibi wameomba maafisa wa serikali kuchukua hatua kabla ya mzozo wa kiafya kuzuka nchini kufuatia mgomo wa wauguzi.

Kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetang’ula, Mwakilishi wa wanawake wa Kakamega Elsie Muhanda na Askofu Rashid Nanjira wa kanisa la Christian Warrior Prayer Ministries walisema, malalamishi ya wahudumu wa afya yanafaa kushughulikiwa upesi ili kuepushia wagonjwa dhiki wanayopitia.

Wahudumu hao waligoma Desemba 8, 2020, wakitaka walipwe marupurupu, wawe na bima ya afya. Pia walilalamikia ongezeko la vifo vya wenzao kwa sababu ya kukosa vifaa vya kujikinga dhidi ya corona.

Bw Wetangula alihimiza serikali kutoruhusu siasa kuvuruga sekta ya afya akiwataja wahudumu wa afya kama wazalendo.

Bi Muhanda alisikitika kuwa mgomo unaoendelea wa wauguzi na wahudumu wengine wa afya umelemaza sekta ya afya kote nchini.

Askofu Nanjira alisema kwamba mgomo huo umeathiri sekta hiyo kwa kuvuruga huduma muhimu kama kiliniki za akina mama wajawazito, chanjo ya watoto na wagonjwa walio na maradhi sugu.

“Tunafaa kuzungumza nao wafute mgomo huu. Wakenya wanakufia ndani ya hospitali kwa sababu hakuna wa kuwahudumia. Huu ni ukatili,” alisema Askofu Nanjira.

Nao viongozi wa dini ya Kiislamu kaskazini mwa Bonde la Ufa waliomba serikali isimamishwe mchakato wa kubadilisha katiba (BBI) ili kushughulikia matakwa ya wahudumu wa afya wanaogoma.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa wahubiri wa Kiislamu eneo la Uasin Gishu Sheikh Abubakar Bini, walisema mamilioni ya Wakenya wanakabiliwa na hatari ya kufariki ikiwa mgomo huo utaendelea.