Habari Mseto

Watalii watakiwa kupanda miti wanapoingia nchini “Mtalii mmoja, Sh20, mti mmoja”

May 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na SINDA MATIKO

KILA mtalii anayeingia nchini sasa atatozwa Sh20 na serikali kupanda miti Kenya.

Mkakati huo umefichuliwa na Waziri wa Utalii Dkt Alfred Mutua alipokuwa akikizungumza kwenye mkeka ulioandaliwa na balozi wa Australia nchini Bi Jenny Da Rin kutangaza ujio wa kampuni kubwa ya utalii kutoka Australia Intrepid.

Kulingana na Mutua, serikali inakuja na mpango kazi ambao utamtaka kila mtalii anayeingia Kenya kutoka pembe yeyote ya dunia, anapanda mti Kenya.

“Mpango kazi wetu kama serikali ni kuhakikisha kwamba kwa kila mtalii, tunapanda mti. Kupitia bodi yetu ya utalii, tayari tumeanza na mchakato ambao kwamba utahakikisha mtalii anapata taarifa kuwa atatakiwa kupanda mti kila anapotua Kenya.” Mutua aliiambia safu hii.

Kulingana na Waziri, idara ya bodi ya Utalii itahakikisha kwamba kila eneo ambapo mtalii ataishi kubuku kama sehemu yake ya malazi, basi patakuwepo na miche ya miti ambayo atakabidhiwa na kuonyeshwa sehemu ya kuipanda.

“Hoteli zote na zile Airbnb watakapoishi kutakuwa na miche hizo atakayopewa mtalii. Na tunasema kwa mpango huo, kutakuwa na ada ndogo ya Sh20 tutakayotoza kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa miche hiyo. Kusudi letu ni kuhakikisha kuwa kwa kila mtalii tunapata mti na hata ikiwezekana wao wenyewe watakuwa wanafuatilia ukuaji wa mti huo kila watakapokuwa wanazuru Kenya tena,” aliongeza Dkt Mutua.

Mutua alitamka hayo huku akiipongeza kampuni ya Interpid kwa mpango wake wa kupanua soko lake kwa kuingia eneo la Afrika Mashariki.
Mwaka jana, kampuni hiyo iliwaleta wageni zaidi ya 5,000 kuzuru maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Intrepid, Darell Wade alisema kuwa malengo yao ni kuongeza idadi hiyo ya wageni na ili kufanya hivyo wameamua kukita kambi zaidi eneo hili.
“Nairobi itakuwa ndio makao makuu yetu tunapolenga kupanua soko letu Afrika Mashariki hasa kwenye mataifa ya Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda,” Wade alisema.