Habari Mseto

Watanzania na Waganda wanashinda Wakenya kwa ulaji tumbaku, ripoti ya WHO yaonyesha

February 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

WAKATI taifa la Tanzania lilikuwa likishughulika kuwania ubingwa wa soka barani Africa, Wakenya walikuwa wakishindana kutumia bidhaa za tumbaku.

Licha ya Tanzania kutimuliwa katika awamu ya makundi katika dimba linaloendelea nchini Ivory Coast hivyo basi kuwa tu miongoni mwa timu 54 bora Afrika, Wakenya wameibuka wa saba katika ulaji ugoro lakini wakiwa nyuma ya Watanzania na Waganda.

Makubwa haya ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Afya duniani (WHO), ubingwa huo ukiwa ni hata kwa watoto wa miaka 15.

Walioibuka kidedea katika ripoti hiyo ni Afrika Kusini wakifuatwa na Algeria huku DR Congo ikiwa ya tatu.

Taifa la Ethiopia lilikamata nafasi ya nne huku Tanzania ikiwa ya Tano nayo Uganda ikiwa ya sita ndio Kenya iwe ya saba.

Ripoti hiyo inasema kwamba Wakenya 3.1 Milioni kati ya wote 50 milioni wanaotumia tumbaku katika utafiti wa hadi mwisho wa mwaka wa 2022, asilimia ya 89 ni wanaume.
Wavutaji wa sigara ndio wengi katika nchini Kenya, WHO ikishikilia kwamba wao ni 2.5 milioni, 108, 000 wakiwa ni wanawake.

Awali, na katika suala hilo hilo la miohadarati, Kenya iliorodheshwa katika nafasi ya sita kuhusu ubingwa wa uvutaji bangi.

Mwanasiasa George Wajackoyah huipigia debe ihalalishwe akisema ni mmea wa faida na ambao unaweza ukasaidia taifa hili kulipia madeni yake katika kipindi kifupi cha baada ya uzinduzi wa kuikuza.

Hata hivyo, msimamo huo wa Wajackoyah haujaungwa mkono na utafiti wowote wa kuaminika huku Wakenya wengi wakimkataa katika azima yake ya kuwa Rais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 ambapo alipata chini ya asilimia moja ya kura.

Kulingana na utafiti wa kitengo cha Afya na Elimu cha Marekani, waliolemea Kenya katika uvutaji wa bangi ni raia wa Nigeria ambapo miongoni mwa raia wkee, watu milioni 20.8  huivuta.

Ethiopia ndio wa pili ambapo raia milioni 7.1 huivuta huku Misri ikiwa na watu milioni 5.9 ambao ni waraibu wa mihadarati hiyo.

Taifa la DR Congo limeorodheshwa la nne Afrika likiwa na wavutaju milioni 5, Tanzania likiwa na wavutaji milioni 3.6 huku Kenya ikiridhika na nafasi ya sita kwa kuwa na waraibu milioni 3.3.

Taifa la Sudan liko katika nafasi ya saba kwa kuwa na wapenda bangi  milioni 2.7 huku taifa la Uganda likiwa na wavutaji milioni 2.6.

Madagascar wako na wapenda bangi milioni 2.1 nao Ghana wakifunga orodha ya kumi bora kwa kuwa na wanabangi milioni 2.

Duniani, Marekani, Canada, Nigeria na Australia raia katika mataifa hayo walirekodiwa kupenda bangi sana hasa katika wale walio na miaka 15 kwenda juu.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya 2021 ilikuwa imeonya kwamba wavutaji bangi Afrika walikuwa wakiongezeka kwa kasi na huenda watinge asilimia 40 kabla ya 2030.

Zimbabwe, Malawi, Niger na Zambia ni mataifa ambayo yamesemwa kuwa na wapenda bangi wachache wakiwa ni milioni 1.1, 1.2, 1.2 na 1.4 mtawalia.

Hata hivyo, ripoti hizo zote zinaonya kwamba uraibu wa bangi ni hatari kwa afya ya watumizi, kusambaratikiwa na akili kukiwa ndio athari kuu.