• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Watanzania walalamika sanamu iliyozinduliwa Ethiopia si sura ya Nyerere!

Watanzania walalamika sanamu iliyozinduliwa Ethiopia si sura ya Nyerere!

NA WANDERI KAMAU

BAADHI ya raia nchini Tanzania wamekosoa vikali sanamu mpya iliyozinduliwa Jumapili katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU),  jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia, kama kumbukumbu kwa rais wa kwanza wa taifa hilo, Mwalimu Julius Nyerere.

Raia hao walisema kuwa sanamu hiyo haifanani na sura ya Mwalimu Nyerere.

Sanamu hiyo ilizinduliwa nje ya makao makuu ya umoja huo.

“Ninajua hiki ni kitendo cha hekima, japo sanamu hii haifanani kwa vyovyote vile na Mwalimu Nyerere (akiwa mchanga au akiwa mzee),” akasema Maria Sarungi kwenye mtandao wa ‘X’.

“Huyu si Nyerere wetu,”akaeleza mtu mwingine.

“Watengeneze sanamu nyingine au waache tu. Hii si sanamu inayofanana na Mwalimu Nyerere hata kidogo. Huenda tunamkumbuka mtu mwingine badala ya Nyerere,” akasema Morrison Musa, kwenye mtandao wa Facebook.

Nyerere alikuwa kiongozi wa Tanzania kati ya 1961 na 1985. Alikuwa kiongozi aliyejitolea kuwapa hifadhi viongozi walioongoza harakati za kuwakabili Wazungu katika mataifa ya kusini mwa Afrika.

Mwaka uliopita, umoja huo ulilazimika kuondoa sanamu nyingine iliyotengenezwa kumkumbuka rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda, baada ya raia wengi wa taifa hilo kulalamika kwamba haikuwa ikifanana naye.

Mwalimu Nyerere alitekeleza jukumu muhimu kwenye harakati za kubuniwa mwa Muungano wa Umoja wa Afrika (OAU) mnamo 1985, ambao baadaye ulibadilishwa kuwa Umoja wa Afrika (AU).

Uzinduzi wa sanamu yake ulihudhuriwa na marais wengi akiwemo mweyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Moussa Faki Mahamat.

Akasema Faki: “Sifa ya kiongozi huyu inaonyesha jinsi Afrika inafaa kuungana na kuwa na sauti moja kwa masuala yanayoiathiri.”

  • Tags

You can share this post!

Director Trevor, Mungai Eve waendelea kuwapa mashabiki...

Mwoshaji choo akemea kipusa kwa kukataa kumsalimia kwa...

T L