Watawa walalamikia visa vya wakongwe kutelekezwa jamaa zao zikihamia mijini
NA WAIKWA MAINA
WATAWA wa Kanisa Katoliki wamelalamikia idadi kubwa ya visa ambapo wakongwe wanatelekezwa na jamaa zao katika kaunti za Nyandarua na Laikipia.
Wakikagua shughuli inayoendelea ya ujenzi wa makazi ya kusitiri wakongwe 80 katika kijiji cha Gatundia, kata ya Rumuruti, Kaunti ya Laikipia, watawa hao walisema hali hiyo inachangiwa na umaskini na mwenendo wa watu kuhamia maeneo ya mijini.
“Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, watu wenye umri mdogo wanaondoka vijijini na kuhamia miji kusaka ajira na katu huwa hawarudi nyumbani. Hali hii huchangia wakongwe kutelekezwa katika kaunti za Nyandarua na Laikipia,” akasema Mtawa Redemptor Ikonga.
“Wengi wa wakongwe hao hupatwa na magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na uzee na mengine sugu haswa kwa wanaoishi katika maeneo baridi. Hiyo ndio maana tuliamua kujenga makazi haya katika eneo la Gatundia ambayo huwa na joto,” akaongeza Mtawa huyo kutoka Muungano wa Watawa wa Congregants of Dimesse Sisters, ambao ndio wafadhili wa mradi huo.
Alisema makazi hayo yatatumiwa kama makao ya wakongwe na kuwapa usalama, utulivu wa kiakili na huduma za kiafya.
Mtawa Ikonga alisema kituo cha St Anne and Joachim Hope Centre kitatoa mahitaji ya kimsingi kwa wakongwe walioko katika kaunti za Nyandarua na Laikipia.
“Mradi huu utakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu kando na kuhudumia wakongwe, pia utawasaidia watoto waliotelekezwa. Makazi haya pia yatatumika kushirikisha mipango ya kutoa lishe, huduma za afya na lishe kwa kwa wakongwe na watoto waliotelekezwa,” akaongeza Mtawa Ikonga.
Kauli yake iliungwa mkoo na mwenzake, Mtawa Agnes Sarange aliyetaja mradi huo kama bora na utakaowasaidia wakongwe katika jamii.