Habari Mseto

Watoto wa kurandaranda waokolewa

August 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

ZAIDI ya watoto 1,400 wa kurandaranda humu nchini walikusanywa, kurekebishwa tabia na kujumuishwa na familia zao tangu Kenya ianze kukabiliwa na janga la corona Machi.

Kulingana na mwenyekiti wa bodi ya Street Families Rehabilitation Trust Fund (SFRTF), Bi Linah Jebii Kilimo, watoto hao wa kurandaranda sasa wanapokea malezi bora kutoka kwa familia zao.

Hata hivyo, Bi Kilimo alieleza namna watoto hao wanaendelea kudhulumiwa kingono, akisema wengi wanalazimika kutumia dawa za kulevya, kujihusisha na sinema chafu na ukahaba wa watoto.

“Waototo wa kurandaranda wanaendelea kudhulumiwa huku haki zao zikikiukwa kutokana na mazingira wanamoishi,” alisema Bi Kilimo alipozuru makao ya watoto wa kurandaranda wanaorekebishwa tabia ya Onesmus Good Boys Centre.

Mkurugenzi wa Onesmus Good Boys Centre Joseph Matheka. Picha/ Winnie Atieno

Hata hivyo, Bi Kilimo aliwasihi wazazi na wale waliotwikwa jukumu la kulea watoto kuhakikisha wanapata malezi bora ili wasitokomee mitaani.

“Wapatie watoto hao mazingira na malezi bora; wale waliorekebishwa tabia nao msiwanyanyapae. Tunajizatiti kuokoa watoto wa kurandaranda ili wajumuike na familia zao,” alisisitiza Bi Kilimo.

Akinukuu ripoti ya kitaifa ya watoto wa kurandaranda, Bi Kilimo alitaja sababu za kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaotokomea kuishi mitaani ikiwemo ufukara, familia kutengana, vita na dhuluma nyumbani kwao, maradhi, malezi mabaya na wengine kuachwa peke yao kujilea.

Hata hivyo, Bi Kilimo alisema watoto hao wanaendelea kupewa mafunzo ili waweze kujikimu kimaisha.

Mkurugenzi wa Onesmus Good Boys Centre Joseph Munyasya Matheka alisema watoto hao hunyanyapaliwa licha ya kwamba ni watoto tu wa kawaida ambao wasipoelekezwa wanapotoka kimaadili, lakini wakipewa ushauri na maelekezo wanakuwa watu wazuri katika jamii.