Habari Mseto

Watoto waliofariki Pumwani kufanyiwa upasuaji

September 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA COLLINS OMULO

UPASUAJI wa kubaini kilichosababisha vifo vya watoto 12 katika hospitali ya kujifungulia akina mama ya Pumwani utafanywa Jumanne.

Naibu mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNHCR) George Morara alisema kuwa upasuaji utafanyiwa katika mochari ya jiji la Nairobi na mwanapatholojia wa serikali na kushuhudiwa na maafisa wa idara ya upelelezi na familia zilizoathiriwa.

“Upasuaji huo utatusaidia kujua iwapo kulikuwa na makosa ya kitaaluma yaliyofanya watoto hao kufariki kwa kulinganisha matokeo tutakayopata na yale ambayo wasimamizi wa hospitali hiyo walitoa,” alisema Bw Morara.

Alisema iwapo ripoti ya mwanapatholojia itafichua kwamba kulikuwa na makosa ya kitaalamu, basi waliohusika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Hospitali ya Pumwani iligonga vichwa vya habari wiki moja iliyopita kutokana na ziara ya ghafla ya Gavana Mike Sonko iliyofichua kwamba asasi hiyo inakabiliwa na shida tele.

Mnamo Alhamisi katibu mkuu wa chama cha wauguzi (KNUN) Seth Panyako alitaka hospitali hiyo kufanyiwa uchunguzi kubaini chanzo kamili cha vifo vya watoto hao akisema idadi ya watoto na akina mama wanaofariki Pumwani inatisha.

Hata hivyo, wasimamizi wa hospitali hiyo wamejitetea na kusema kuwa hakuna anayefaa kulaumiwa kutokana na vifo hivyo. Msimamo wao ulifanya Gavana Sonko kuwasimamisha kazi pamoja na maafisa wanne wakuu wa serikali ya kaunti waliowaunga mkono.

Ripoti ya awali iliyotayarishwa na Bodi ya Madaktari na Wataalamu wa Meno (KMPDB), watano kati ya watoto hao waliokuwa wamelazwa katika kitengo cha watoto wanaozaliwa walikufa kutokana na sababu ambazo hazikueleweka.

Afisa Mkuu Mtendaji wa bodi hiyo Daniel Yumbya, alisema watoto wote walikufa kati ya Septemba 12 na 17 na kwamba watatu walizaliwa wakiwa wamekufa na wanne walikufa saa 24 baada ya kuzaliwa.

Gavana Sonko alisema alizungumza na hospitali ya Aga Khan ambayo ilikubali kutoa madaktari zaidi, wauguzi na wafanyakazi kuhudumu Pumwani kwa miaka miwili bila malipo yoyote.

Wakati huo huo, Gavana Sonko ametangaza mipango ya kuipa hospitali ya Pumwani sura mpya anayosema itasuluhisha matatizo yote katika hospitali hiyo.

Sonko ana mpango wa kujenga hospitali mpya ya Pumwani yenye vitanda 450.

Alisema hospitali hiyo mpya itakuwa ikitoa huduma za upasuaji, chanjo, matibabu na huduma za dharura kwa saa 24.

“Hospitali mpya ya Pumwani itakayokuwa na orofa 10 itakuwa karibu na ya sasa, itakuwa na kitengo cha kutoa matibabu kwa watoto mahtuti, kitengo sawa cha watu wazima, nyumba za wafanyakazi na vifaa vyote vinavyohitajika,” Bw Sonko alisema Ijumaa.

Alisema ujenzi wa hospitali hiyo mpya utapunguza msongamano katika hospitali ya sasa ya Pumwani.