• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Watoto waliotoweka wakiwinda Lamu hatimaye wapatikana

Watoto waliotoweka wakiwinda Lamu hatimaye wapatikana

Na KALUME KAZUNGU

WATOTO wanane waliokuwa wameripotiwa kutoweka nyumbani kwao tangu Jumapili asubuhi wakiwa katika shughuli za kuwinda tumbiri eneo la Kizingitini, Kaunti ya Lamu hatimaye wamepatikana.

Watoto hao wa kati ya umri wa miaka tisa na 13 walikuwa wameondoka nyumbani kwao majira ya saa tatu asubuhi na na kuelekea Mabiu Kivonga ambalo ni eneo la msitu wa mikoko kwa minajili ya kuwinda tumbiri na ndege.

Aidha wazazi wa watoto hao walianza kushikwa na wasiwasi pale watoto hao walikosa kurudi nyumbani siku yote ya Jumapili.

Iliwalazimu wazazi kuwatafuta watoto hao bila mafanikio, hivyo wakalazimika kupiga ripoti kwa polisi Jumatatu asubuhi ili kusaidiwa kuwatafuta watoto hao.

Mzee wa kijiji cha Kizingitini, Bw Kassim Shee ameambia Taifa Leo kwamba ni mara ya kwanza kwa watoto hao kuingia msituni kuwinda na kisha kukosa kurudi nyumbani.

“Wao huwa kila mara wanaingia msituni kuwinda tumbiri na ndege na kisha kurudi mapema walikotoka. Wasiwasi ulitanda kijijini hapa baada ya watoto kukosa kurudi nyumbani mchana kutwa na pia usiku kucha. Hii ndiyo sababu tukaamua kuripoti kwa kituo cha polisi hapa Kizingitini,” akasema Bw Shee.

Katika mahojiano Jumatatu, Afisa Mkuu wa kituo cha polisi cha Kizingitini, Bw Emmanuel Okanda, amethibitisha kupatikana kwa watoto wote wanane wakiwa hai.

Bw Okanda amesema watoto hao walipotea njia wakiwa msituni, hivyo kuishia kulala msituni.

“Watoto wamepatikana wakiwa buheri wa afya. Walikuwa na mbwa wao na vifaa vingine vya kuwindia wanyama. Walituarifu kuwa walikuwa wamepotea njia msituni. Ni wavuvi ndio waliowaona watoto hao kwenye kisiwa cha mbali leo asubuhi na kuwachukua kuwarudisha Kizingitini. Tayari tumewakabidhi watoto wote kwa wazazi wao,” amesema Bw Okanda.

Watoto waliokuwa wametoweka nyumbani ni pamoja na Omar Mshamu wa umri wa miaka 13, Fahad Bunu (10), Sudeysi Turuba (9), Bablii Kibwana (13), Murshid Ibrahim (10), Hossein Miruwa (11), Aboud Abuu (9) na Shelali Nyasumani Hamadi (12).

Wazazi watakiwa wawe mstari wa mbele

Mmoja wa wazee wa Kizingitini, Bw Khaldun Vale amewataka wazazi kuwa mstari wa mbele katika kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kuepuka watoto hao kutumiwa na watu wabaya.

“Shughuli za kuwinda zilikuwa zikifanywa kitambo na jamii yetu ya Kibajuni. Cha msingi ni kwamba miaka ya sasa imebadilika. Ni vyema ikiwa wazazi watawahimiza watoto wao kusoma ili wawe raia wema siku za usoni. Kuwaacha watoto kiholela ni makosa kwani huenda wakaishia mikononi mwa watu wabaya, ikiwemo walanguzi wa dawa za kulevya na hata magaidi,” amesema Bw Vae.

  • Tags

You can share this post!

Ushahidi waanikwa mahakamani jinsi wakili Willie Kimani...

Korti yaagiza ukaguzi KTDA baada ya kilio cha wakulima

adminleo