Habari Mseto

Watu 20 waponea kifo baada ya chombo cha majini kuzama Ziwa Victoria

May 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WATU 20 wameponea kifo baada ya kuokolewa kutoka chombo cha usafiri wa majini ambacho kilizama katika Ziwa Victoria Jumamosi.

Walikuwa wakisafiri kutoka kisiwa cha Mageka hadi ufuo wa Usenge katika kaunti ndogo ya Bondo, ajali hiyo ilipotokea.

Kulingana na Chifu wa Mageta Ambrose Ogema, injini ya boti hiyo ilipataka hitilafu ya kimitambo karibu na Kisiwa cha Sirigombe.

Aliwaambia wanahabari kwamba abiria hao ambao walikuwa wakisafiri kwenye boti zingi walifika haraka kuwaondoa abiria hao ambao walikuwa wamevalia jaketi za usalama.

Baadaye walipelekewa katika ufuo wa karibu wa Kabarua na wengine wakapelekwa katika Zahanati ya Mageta kwa ukaguzi wa kiafya.

Mnamo Ijumaa, Uganda ilionya kuhusu ongezeko la viwango vya maji katika Ziwa Victoria kwa kiasi kikubwa zaidi katika kipindi cha miaka 50.

Hii ni baada ya mvua kunyesha kwa wingi katika maeneo ya karibu na Ziwa hilo mfululizo kwa miezi minane.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari baadhi ya hoteli maarufu nchini Kenya kama vile Protea Hotel, inayomilikiwa na Shirika la Kustawisha Utalii Nchini (TPC) imefunikwa na maji.

Waziri wa Maji na Mazingira Sam Cheptoris pia alisema kuwa hali hiyo itaathiri shughuli za viwanda vya uzalishaji umeme nchini Uganda.