• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 11:29 AM
Watumiaji mitandao ya kijamii wakashifu hatua ya Miguna kuzuiwa kuabiri ndege

Watumiaji mitandao ya kijamii wakashifu hatua ya Miguna kuzuiwa kuabiri ndege

Na SAMMY WAWERU

HISIA mseto zimetolewa na Wakenya wakiwemo watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii kufuatia madai kuwa wakili Joshua Miguna Miguna amezuiwa kuabiri ndege ya shirika la Lufthansa, Frankfurt, Ujerumani ambapo alitarajiwa kurejea nchini.

Miguna alifurushwa nchini mwaka 2018 na juhudi zake kurudi ziligonga mwamba pale alihangaishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Mtumiaji mmoja ameshangazwa na hali mkanganyiko na drama zilizoshuhudiwa licha ya serikali Jumatatu kusema haikutarajia purukushani.

“Kwa nini kumhangaisha kiasi hicho? Idara ya uhamiaji ilikuwa imeahidi kufanikisha safari yake nchini. Kumbe ni mchezo wa basketiboli kwenye uga wa soka,” amechapisha Joyce Gichuhi, kufuatia masaibu yanayomzingira kiongozi huyo aliyethubutu kujitangaza kiongozi wa vuguvugu la NRM na lililopigwa marufuku na serikali.

Ronald Langat ameishutumu serikali kwa hatua hiyo, akidai inajishughulisha kuhujumu raia halali wa Kenya.

“Inajua kuzuia Miguna Miguna lakini hailindi wananchi dhidi ya mashambulizi ya al-Shabaab,” asema Langat.

“Kwa nini anyimwe haki yake kikatiba kuwa nchini? Serikali ya hujuma tu,” amechapisha Japheth Kivuitu.

Shaky Maina anaicharura serikali, “Wakenya wanaoshangilia kuzuiwa kwa Miguna Miguna, serikali iyo hiyo ndiyo itaiba na kufuja mali ya umma iyatumie kufanya maendeleo hewa na kuagiza bidhaa bandia,” akisisitiza wananchi wanapaswa kufumbua macho.

Kwenye mitandao, wakili huyo amekuwa akichapisha maandalizi yake kurejea nchini kufuatia agizo la mahakama kuu. Alitarajiwa kusafiri leo, na kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA, jijini Nairobi mwendo wa saa tatu na dakika ishirini na tano jioni.

Hata hivyo, Jumanne asubuhi kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Hot96 FM kwa simu, Miguna alisema shirika la ndege la Lufthansa limemzuia kusafiri kutoka Frankfurt, Ujerumani, kwa kile anadai kama ilani kutolewa asirudi Kenya wala taifa lolote katika Bara la Afrika.

“Niko katika uwanja wa Lufthansa na wanasema idara ya usalama Kenya imenizuia kurejea Kenya. Inasema serikali ya Kenya imeagiza nirudishiwe ada ya usafiri na kwamba nisiruhusiwe kutua nchi yoyote Afrika,” akanukuliwa wakili huyo.

Aliendelea kueleza kwamba shirika hilo la ndege linasema sharti serikali ya Kenya itume ujumbe kufuta ilani iliyotolewa ili aruhusiwe kuabiri ndege.

Muda na saa ya kutoka Ujerumani

Kwa mujibu wa maelezo ya Dkt Miguna kwenye chapisho lake mitandaoni, alipaswa kuondoka Ujerumani Jumanne saa tano na dakika ishirini asubuhi na kutua JKIA saa tatu na dakika ishirini na tano jioni.

Baadhi ya Wakenya hata hivyo, wanahisi wakili Miguna Miguna alipaswa kupanga safari yake kisiri. “Jenerali ninakushauri upange mambo yako kwa siri,” anasema Abas Njuguna, na katika uo huo Nicholas Kitonga akitaka majibu kwa nini azuiwe kurudi alikozaliwa.

Abednego Malia amezua utani, ‘akishangaa’ kitakapopelekwa chakula alichoandaliwa kumkaribisha.

“Tumemuandalia mapochopocho ya mlo, tutaupeleka wapi?” akatania.

Msemaji wa serikali Kanali mstaafu Cyrus Oguna amesema Miguna yuko huru kuingia nchini, kupitia hakikisho la Rais Uhuru Kenyatta. Amesema idara ya uhamiaji itashughulikia ilani inayosemekana kutolewa.

Dkt Miguna ambaye aliwania kiti cha ugavana Nairobi 2017, ingawa hakufua dafu, alifurushwa nchini mara ya kwanza Februari 7, 2018. Juhudi zake kurejea nchini Machi 28 mwaka huo hazikufanikiwa. Ana uraia wa mataifa mawili, Kenya na Canada.

Aidha, masaibu yake yalianza alipomuapisha kiongozi wa ODM Raila Odinga kama ‘Rais wa Wananchi’. Bw Odinga kwa sasa anashirikiana na serikali ya Jubilee sako kwa bako, baada ya salamu za maridhiano Machi 2018, maarufu kama ‘Handisheki’.

You can share this post!

Serikali yakanusha madai kwamba imeshindwa kuingiza ARVs...

Kenya nambari tatu ulimwenguni nchi zenye idadi kubwa ya...

adminleo