Habari Mseto

Watumizi wa mafuta taa nchini wapungua kwa 75%

October 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

MATUMIZI ya mafuta taa yamepungua kwa asilimia 75 baada ya serikali kuongeza ushuru kwa bidhaa hiyo kwa Sh18 kwa lita moja.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC).

Kulingana na mkurugenzi wa ERC Pavel Oimeke, upungufu huo umetokana na kupungua kwa mahitaji ya mafuta ya taa miongoni mwa wafanyibiashara waliokuwa wakinunua kuyachanganya na petroli au dizeli kwa lengo la kujipa mapato zaidi.

“Kiwango cha mafuta taa ambacho kinachukuliwa katika depo kimepungua sana. Kulingana na utafiti wetu, asilimia kati ya 70 na 75 ya mafuta taa yaliyokuwa yakinunuliwa yalikuwa yakitumiwa kuchanganya na petroli au dizeli,” alisema.

Kuchanganywa kwa mafuta hufanya injini kuharibika na upungufu wa mapato kwa upande wa serikali.

ERC imekuwa ikitekeleza operesheni ya kuwakamata wote wanaopatikana wakiuza mafuta yaliyochanganywa.

Katika muda wa miezi mitatu, ERC imewakamata wafanyibiashara kama hao maeneo tofauti nchini ikiwemo Nairobi, Eldoret, Kisumu na Nakuru.