Wauguzi waitiwa kazi 2,500 nchini Saudia
NA LABAAN SHABAAN
KUNA nafasi 2,500 za kazi katika sekta ya afya Saudi Arabia ambazo Wizara ya Leba inawahimiza Wakenya kutuma maombi.
“Serikali ya Kenya inashirikiana na Ufalme wa Saudi Arabia ili kuimarisha uhamiaji wa kikazi kwa usalama, mfululizo na ufanisi kati ya nchi hizi mbili,” ilisema notisi iliyotiwa saini na Katibu wa Wizara Shadrack Mwadime.
Rais William Ruto amekuwa akikashifiwa kwa ziara mfululizo nje ya nchi wakati hali ngumu ya uchumi inakabili taifa.
Kama mjibizo kwa shutuma hasaa kutoka kwa Upinzani, Rais amesema ziara hizi zinavunia Wakenya nafasi za kazi ili wajitegee uchumi ughaibuni na kuimarisha Mapato ya Taifa (GDP).
Watakaofaulu kuwahi kazi hizi watapata mikataba ya miaka miwili wakifanya kazi saa nane kwa siku.
Kutegemea viwango vya elimu, mishahara itakuwa kati ya Sh92,000 na Sh147,670 kwa mwezi.
Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed amesema zaidi ya nafasi za kazi 300,000 zitatangazwa kwa Wakenya ifikapo Machi 2024.
Bw Hussein anafafanua kuwa kazi hizi za sekta mbalimbali ziko katika mataifa ya Ujerumani, Urusi, Israeli, na Serbia.
Wanaonuia kuajiriwa ughaibuni wanahitajika kuzuru wavuti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira (National Employment Authority).