Waume waambia wenzao wakome kulamba asali kiholela
Na Charles Wanyoro
WAFANYABIASHARA vijana Kaunti ya Embu wamesikitishwa na ongezeko la visa vya kuwatelekeza watoto eneo hilo na wakawashauri wanaume wenzao wakome kulamba asali ovyoovyo.
Kupitia chama chao cha ‘Timu Kali’ wafanyabiashara hao walisema idadi ya watoto wanaorandaranda mitaani na ombaomba imeongezeka baada ya wengi wao kupuuzwa na wakawataka wanaume kuwa msitari wa mbele kukabiliana na tatizo hilo.
Wakiongozwa na Bw Charles Ndirangu na Bw Emilio Mungatana, wanaume hao waliwashauri wenzao kutozaa watoto ambao hawana nia ya kulea ili kupunguza visa hivyo.
Walikuwa wakizungumza katika makao ya watoto ya Child Welfare society of Kenya yanayosimamiwa na Dayosisi ya Embu ambapo waliwatembelea watoto 45. Waliwataka viongozi kuzungumzia hadharani suala hilo.
“Inasikitisha kwa sababu watoto hawa hawako hapa kwa bahati mbaya. Walizaliwa na wanaume na wanawake ambao wako eneo hili, baadhi wana wazazi lakini waliwatelekeza. Viongozi wa kidini na wale wengine wanafaa kuzungumza na wazazi ili waweze kuwajibika,” alisema Bw Ndirangu.