Waumini 100 waabudu kando ya barabara
Na FRANCIS MUREITHI
WAUMINI wanaozi 100 wa Kanisa la Word of Faith lililo katika mtaa wa mabanda wa Kaptembwa, Nakuru Magharibi, walilazimika kufanya ibada yao kando ya barabara Jumapili baada ya kanisa lao kufungwa kufuatia mzozo na kanisa lingine.
Idara ya kutatua mizozo ya kodi ilifunga kanisa hilo baada ya kanisa jirani la Independent Gospel Missions of Kenya, kudai kuwa ndilo mpangaji mpya wa ardhi hiyo.
Pasta Henry Ambeva, alisema waumini walishtuka walipokuta wamefungiwa kanisa kwani walikuwa wamelipa kodi ya Sh33,000 inayohitajika kila mwaka kwa mwenye ardhi.
“Tuna mkataba na mmiliki wa ardhi hii na tulishangaa kwamba idara ya kutatua mizozo ya kodi ilishirikiana na mmiliki huyo kutufurusha kutoka kwa ardhi ya kanisa letu licha ya kuwa na mkataba wa miaka mitatu ambayo ilifaa kukamilika mwaka wa 2020,” akasema Bw Ambeva.
Kulingana na maafisa wa kanisa hilo, mmiliki wa ardhi anadai kwamba kanisa halikukamilisha kodi ya mwaka huu. Lakini Bw Ambeva alikanusha madai hayo na kusema mwenye ardhi alidai kuuza ardhi hiyo.
“Tulikuwa na maelewano yaliyotiwa sahihi katika afisi ya chifu na hivyo basi idara ya kutatua mizozo ya ardhi inafaa ijitokeze wazi kutoa uamuzi wenye haki badala ya kupendelea upande mmoja,” akasema Bw Ambeva.