Habari Mseto

Waumini saba wafa katika ajali wakienda kulipa mahari Kitui

April 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

PIUS MAUNDU na GEORGE SAYAGIE

WAUMINI saba wa kanisa moja jijini Nairobi waliokuwa wakienda kwa sherehe ya kulipa mahari, walikuwa miongoni mwa watu 11 waliofariki jana kwenye ajali mbili tofauti.

Watu hao saba waliaga dunia wakati gari walilokuwa wakisafiria kutoka Nairobi kuelekea Kitui, lilipobingiria mjini Ikutha, katika barabara ya Kibwezi na Kitui. Wengine wanne walikufa kwenye ajali iliyotokea Narok.

Waliofariki kwa ajali ya Kitui ni pamoja na mchungaji wa Kanisa la Glory Celebration Center, Kayole na mtoto walioaga dunia papo hapo. Manusura walitibiwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Ikutha, Kaunti ya Kitui.

“Tulipokea wagonjwa 11 hospitalini. Wawili waliaga dunia kutokana na majeraha waliyopata kutokana na ajali hiyo. Tunataka kuwapeleka wagonjwa wawili ambao wamo katika hali mbaya hadi Hospitali ya Kitui. Tunashughulikia wagonjwa wengine ambao hali yao ni dhabiti,” alisema mkuu wa hospitali hiyo, Dkt Paul Kibati.

Gari hilo lenye nafasi za abiria 10, lilikuwa limekodishwa kutoka kwa kampuni ya 7UP CBO na lilikuwa kati ya magari kadhaa yaliyokuwa yamekodishwa na kuondoka Nairobi mwendo wa saa tisa kuelekea kwa tamasha hiyo iliyokuwa katika kijiji cha Kwa Mbaki, Kaunti ya Kitui.

“Mpango ulikuwa ni kufika kwa sherehe hizo na kuhudhuria ibada kanisani eneo hilo. Gari hili lilikuwa likiendeshwa kwa kasi, lilibingiria mara tatu na tulimpoteza mchungaji mkuu na wanachama wengine,” alisema Bw Martin Mbuthia katika Hospitali ya Ikutha ambako alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Maafisa wa polisi katika eneo la ajali waliambia Taifa Leo kuwa dereva wa gari hilo alishindwa kudhibiti gari hilo baada ya gurudumu moja la nyuma kupasuka na kusababisha ajali hiyo.

Miili ilisafarishwa na kupelekwa katika mochari ya Ikutha.

Kwingineko, polisi kaunti ya Narok wanamtafuta dereva wa gari la abiria 14 lililoua watu wanne na kusababisha majeraha ya wengine sita baada ya kugongana na gari la kibinafsi katika barabara ya Narok-Bomet.

Gari hilo la uchukuzi wa umma, lilikuwa likisafirisha abiria kutoka Kilgoris hadi mjini Narok lilipogongana na gari aina ya Toyota Prado Jumapili asubuhi katika soko la Katakala, Kaunti Ndogo ya Narok Kaskazini.

Wanne ya waliokuwa ndani ya gari hilo linalosimamiwa na Super Premium Sacco, ambao ni wanawake wawili, mwanamume mmoja na mtoto, waliaga dunia papo hapo.

Watu sita miongoni mwao mtoto wa miaka 11, waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Narok.

Dereva huyo, ambaye kwa sasa hajatambulishwa alitoroka kutoka eneo la ajali dakika chache baada ya ajali hiyo kutokea.

Kulingana na kamanda wa polisi Kaunti ya Narok, Bw Adan Yunis, ajali hiyo ilitokea baada ya gari hilo lililokuwa limebeba watu 10, kugonga gari la kibinafsi kabla ya dereva kupoteza mwelekeo na kuondoka barabarani.