• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Wauzaji pombe bila leseni Juja waonywa

Wauzaji pombe bila leseni Juja waonywa

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu imeanza msako mkali na kuwanasa wauzaji pombe wasio na leseni na hawafuati maagizo ya Covid-19.

Afisa mkuu wa kaunti ndogo ya Juja, Bi Selina Muriithi, alisema hatua hiyo ni ya kuzuia kuenea kwa Covid-19 kwa sababu wengi eneo hilo wanapuuza masharti ya Wizara ya Afya.

“Wakati huu hasa wa siku kuu tutashirikiana na polisi ili kuendesha msako mkali wa kukabiliana na watu wanaokiuka sheria za afya,” alisema Bi Muriithi.

Alisema kwa muda mrefu wauzaji wa pombe kwenye baa wamekosa kufuata sheria zilizowekwa za afya licha ya kupewa onyo kila mara.

“Utapata wateja walio pale wanapitisha muda wao humo huku wakikosa kufuata sheria za afya,” alisema Bi Muriithi.

Aliyasema hayo mnamo Jumatano alipofanya mkutano na wauzaji wa pombe kutoka eneo la Witeithie, kaunti ndogo ya Juja.

“Wafanyabiashara wa pombe ambao hawajakata leseni ya mwaka huu wa 2020 hawatakubaliwa kuendesha biashara zao ifikapo Januari 2021. Watalazimika kulipa faini hiyo kabla ya kupewa leseni nyingine,” alisema afisa huyo.

Alisema yeyote anayeuza pombe rejareja hataruhusiwa bali ni wale wa jumla ndio watapata nafasi.

Hata hivyo wafanyabiashara wa pombe kwa kauli moja walisema watashirikiana na Kaunti ya Kiambu na walinda usalama ili kuona ya kwamba kuna uhusiano mwema.

Afisa wa polisi wa Juja Bw Martin Murimi na chifu wa eneo hilo Bw Muchui Muiruri, walisema kuwa wauzaji wa pombe wanastahili kufuata sheria zote za afya zilizowekwa.

“Sisi kama wafanyakazi wa serikali hatutasita kumchukulia hatua mtu yeyote anayekiuka sheria zilizowekwa na serikali,” alisema Bw Murimi ambaye ni afisa wa polisi eneo la Witeithie.

MCA wa eneo la Witeithie Bw Julius ‘Taki’ Macharia, alisema wafanyabiashara wengi waliathirika na kuenea kwa Covid-19 baada ya biashara zao nyingi kuporomoka.

“Tunaiomba serikali ya Kaunti ya Kiambu kufanya hima kuona ya kwamba wafanyabiashara hao wanapewa mwongozo na usaidizi ili kupanua biashara zao tena,” alisema Bw Macharia.

“Nimejaribu kushauriana na wafanyabiashara wachache na kugundua ya kwamba wengi walifunga kila kitu na hawana la kufanya,” alisema Bw Macharia.

You can share this post!

West Brom wamteua Sam Allardyce kurithi mikoba...

Lewandowski afikisha mabao 250 kwenye Bundesliga