Habari Mseto

Wavinya: Nilimkasirikia Mungu mume wangu mpendwa Henry Oduwole alipofariki

February 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

GAVANA wa Machakos, Wavinya Ndeti ameelezea jinsi alivyomkasirikia Mungu wakati mume wake alipoaga dunia.

Bi Ndeti asema hasira zilimjaa wakati wa kifo cha mume wake Dolamu Henry Oduwole kwa kumuacha akiwa mchanga.

Akizungumza mbele ya umati katika hafla ya mazishi ya mama mkwe wa Naibu Gavana Kaunti ya Machakos Francis Mwangangi, Bi Ndeti alieleza jinsi alihuzunika na kuchanganyikiwa kutokana na uchungu wa kuachwa akiwa mdogo.

“Yule hajawahi kuachwa hajui. Mnavyojua, nilipoteza mume wangu mpendwa 2016. Mimi nilikuwa mchanga, unajua ukiwachwa ukiwa mdogo, unafikiria mambo mengi sana hata nikakasirika na Mungu. Nilimuuliza kwa nini alimchukua mume wangu?” alisimulia Bi Ndeti.

Wakati huo, Bi Ndeti alianza kufungua vifungu vya Biblia ambavyo vingempa majibu ya maswali aliyokuwa nayo kwa Mungu wake.

“Nilifungua Biblia na kupelekwa kwa kitabu cha Ezekia na Yeremia. Jua tu kuanzia leo kwamba mjane si mjane tu. Naamini Mungu atasimama kwa ajili yako na kukuonyesha njia. Usianze kuuliza maswali. Mungu atakupa amani,” Bi Ndeti aliwatia moyo wafiwa.

Mama huyo wa watoto watatu alitaka Naibu wake na mkewe kuwa hodari na kuficha huzuni yao mbele ya wanao.

“Kwa watoto si rahisi kumpoteza mzazi, jifungie chumbani na kulia, msilie mbele ya watoto wenu. Ukiwa mbele ya watoto wako pia utawafanya washuke moyo. Nilikuwa nikijifungia chumbani kwangu na kulia kwa sababu ni lazima uiondoe kwenye mfumo wako,” alisema Bi Ndeti.

Mwaka 2016, bosi huyo wa Machakos alimpoteza mume wake Dolamu Henry Oduwole katika Hospitali ya Nairobi kutokana na saratani ya utumbo.

Katika ukurasa wake wa Facebook wakati huo, Septemba 2016 alipakia ujumbe kufahamisha ulimwengu kuhusiana na kifo cha mumewe.

“Nina huzuni kubwa kutangaza kifo cha mume wangu mpendwa, Dolamu Henry Oduwole, aliyefariki mapema leo asubuhi. Alipigana vita kishujaa na kama familia, tunaomba Mungu atupe nguvu za kuvumilia msiba huu mzito. Mungu ajalie familia yangu nchini Kenya na Nigeria, marafiki zetu, washirika wetu na watu wa Machakos kutupa mkono wa faraja katika kipindi hiki kigumu. Pumzika vizuri Mpenzi wangu, hadi tukutane tena,” alipakia Bi Ndeti, Septemba 26, 2016.