• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Wavuvi hatarini kunyimwa kibali kwa kupuuza kanuni

Wavuvi hatarini kunyimwa kibali kwa kupuuza kanuni

Na MAUREEN ONGALA

MAELFU ya wavuvi katika Kaunti ya Kilifi wapo katika hatari ya kupigwa marufuku kuendeleza shughuli zao iwapo hawatatii kanuni mpya za uvuvi zilizoanza kutekelezwa miaka minne iliyopita kufikia Oktoba mwaka huu.

Sheria hiyo ilifutilia mbali matumizi ya nyavu za kuwanasa samaki wadogo na inawahitaji wavuvi wavae magwanda ya uvuvi pamoja na vifaa vya kisasa vinavyostahili kabla kupewa leseni za uvuvi.

Mnamo Jumatatu, mamia ya wavuvi ambao walikuwa wamekongamana kupata utatuzi kuhusu maswala yanayowakabili, waliiomba serikali kuu kuongeza muda wa makataa ya Oktoba ili kuwaruhusu kupata leseni mpya ndipo watimize sheria mpya.

Wengi wao walihofia kwamba, sheria hizo zitawazuia kuendelea na uvuvi kwa sababu hawana fedha za kununua magwanda na vifaa vinavyotakikana.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Muungano wa waendeshaji wa maboti Shallo Issa, wavuvi hao waliilia serikali ya kaunti iingilie kati suala hilo na kuwanunulia maboti na neti zinazohitajika kabla shughuli zao za uvuvi kupigwa marufuku katika bahari Hindi.

“Wengi wa wavuvi wetu wanatumia neti na maboti ambayo yamepigwa marufuku na serikali. Sheria kwa sasa inaendelea kutekelezwa na hiyo ina maana kwamba, tumefungiwa nje kujitafutia riziki,” akasema Bw Issa.

Afisa huyo alisema wavuvi wanaoendesha shughuli zao kwenye bahari Hindi wamepata pigo kwa sababu hawana njia zozote za kujitafutia riziki.

“Zaidi ya asilimia 95 ya wavuvi karibu na bahari Hindi wamekuwa wakitumia neti zao za zamani baharini. Hii sheria italemaza uwezo wa kiuchumi wa wavuvi wengi ambao hawawezi kununua vifaa vinavyohitajika. Familia kadhaa zitaumia sana,” akaongeza Bw Issa huku akisisitiza wavuvi wengi watakamatwa kwa kuwa watashawishika kuingia baharini ili kupata fedha za kuzikimu familia zao.

Msimamizi wa fuo za Kilifi ya Kati (BMU) Mzee Robinson Shikari naye alisema wavuvi wengi ambao hawana maboti ya kuingia kilomita kadhaa ndani ya bahari wamelazimika kutumia neti zinazowanasa samaki wadogo kinyume cha sheria.

Neti mpya ya kisasa kulingana naye inagharimu Sh23,000 huku boti la kisasa lenye injini likigharimu Sh185,000.

You can share this post!

UNHCR yapinga hatua ya TZ kutimua wakimbizi wa Burundi

Hofu maiti 97 zisizotambuliwa kutapakaa Mbagathi Hospital

adminleo