• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Wawili wafa kimbunga Ialy kikiharibu majengo Pwani

Wawili wafa kimbunga Ialy kikiharibu majengo Pwani

JURGEN NAMBEKA NA MAUREEN ONGALA

WATU wawili wamethibitishwa kufariki baada ya kimbunga Ialy kuvamia ukanda wa Pwani mnamo Jumanne.

Watu wengine sita walipata majeraha na baadhi yao bado wamelazwa hospitalini.

Kimbunga hicho ambacho kilikuwa kimekolea kutokana na dhoruba ya kitropiki Jumanne kilisababisha upepo mkali, mvua na mawimbi mazito katika Bahari Hindi.

Polisi katika Kaunti ya Kilifi walithibitisha kifo cha mtoto wa umri wa miaka minne baada ya upepo mkali kupeperusha paa la darasa la chekechea, huku mfanyakazi katika bohari lililo katika kaunti hiyo akifariki wakati alipokuwa akipokea matibabu ya majeraha aliyopata ukuta ulipoangushwa na upepo.

Kulingana na ripoti ya polisi iliyoonwa na Taifa Leo, upepo huo mkali ulioshuhudiwa Jumanne, ulibomoa ukuta wa bohari la kampuni ya Salima Gasses, ambapo mitungi ya gesi ilikuwa ikihifadhiwa.

Wafanyakazi wawili walipata majeraha kutokana na mawe yaliyoanguka na mmoja wao akafariki katika hospitali ya kaunti ndogo ya Rabai, Kilifi. Mfanyakazi huyo mwingine alitumwa kutafuta matibabu zaidi katika hospitali kuu jijini Mombasa.

Tukio lingine liliripotiwa kwenye kijiji cha Gogoraruhe, kata-ndogo ya Mbalamweni, Kayafungo, Kaunti ya Kilifi. Kimbunga hicho kiling’oa paa la shule ya chekechea ya Msikiti wa Gogoraruhe na kuwajeruhi wanafunzi watano.

Wanafunzi hao walikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Mariakani kwa matibabu, ambapo mwanafunzi wa kike wa miaka minne aliaga dunia kutokana na majeraha akipokea matibabu.

Wanafunzi waliobaki wanne walijeruhiwa vichwani na miguuni na walikuwa wakiendelea kutibiwa.

Tukio hilo linachunguzwa na maafisa wa polisi katika kituo cha polisi cha kaunti ndogo ya Kaloleni, Kilifi.

Naibu kamishna wa Kilifi Kaskazini, Bw Samuel Mutisya alithibitisha kuwa upepo mkali ulikuwa umeathiri shule kadhaa katika kaunti hiyo.

“Upepo umeng’oa mapaa ya shule kadhaa na tunawaomba walimu wasiwaruhusu wanafunzi kusoma katika madarasa yenye mapaa yanayoning’inia,” akasema Bw Mutisya na kuwaomba walimu kuwa waangalifu wanapowaruhusu wanafunzi kuenda nje kucheza ili kuepuka ajali zozote.

Upepo huo ulioshuhudiwa katika eneo la Pwani, uliwaacha wakazi bila huduma muhimu kama vile muunganisho wa umeme na maji.

Kupitia kwa taarifa rasmi kwa wateja, taasisi ya kusambaza maji ya CWDA ilitaarifu umma kuwa kulikuwa na hitilafu katika usambazaji wa huduma za maji katika kaunti za Kilifi na Mombasa.

Kukatizwa huko kwa usambazaji kwa mujibu wao , kulisababishwa na hitilafu za umeme zilizotokana na kuharibiwa kwa nyaya za umeme na miti iliyoanguka.

Katika taarifa hiyo, mtambo wa maji wa Baricho ulikuwa ukipokea umeme wenye nishati ya chini kutoka saa 10 Jumanne na kusababisha hitilafu katika usambazaji wa maji.

Kufikia Jumatano mchana, sehemu kadhaa za Mombasa na Kilifi hazikuwa na umeme.

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro aagiza kufungwa kwa chekechea zote Kilifi...

Mvua bado ipo!

T L