Wawili watiwa mbaroni kwa kuangamiza msichana na kujeruhi dadake Kisii
NA WYCLIFFE NYABERI
POLISI eneo la Nyamache, Kaunti ya Kisii wamewatia mbaroni washukiwa wawili waliovamia nyumba ya Bw Orenge Nyabuto na kumuua bintiye na kumwacha mwingine akiwa na majeraha mabaya.
Bintiye anapokea matibabu katika Hospitali ya Kimisheni ya Tabaka.
Kisa hicho kilitokea katika Kijiji cha Omosaria katika eneobunge la Bobasi usiku wa manane ya Jumapili, April 7, 2024.
Kulingana na Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Nyamache Kipkemboi Kipkulei, washukiwa hao walivamia boma la Bw Nyabuto mwendo wa saa tisa na nusu hivi asubuhi.
Walipata binti zake wawili, wenye umri wa miaka 16 na 9 wakiwa usingizini.
Bw Nyabuto na mkewe hakuwa nyumbani.
Mke wake alikuwa amekwenda kuhudhuria maombi ya mkesha katika kanisa analolishirik, ilhali Bw Nyabuto alikuwa pahala pake pa kazi mbali na nyumbani.
Walipofahamu wazazi hawapo nyumbani, watu hao walivamia watoto hao na kuanza kuwashambulia.
“Binti wa miaka 16 alijeruhiwa vibaya, huku wa miaka tisa 9 akiaga dunia kutokana na majeraha aliyopata,” Bw Kipkulei aliambia Taifa Dijitali kwa njia ya simu.
Aliongeza, “Kulikuwa na povu lililokuwa likitoka mdomoni mwa msichana aliyefariki alipokuwa akipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na maafisa wetu”.
Mkuu huyo wa polisi aliongeza kuwa maafisa wake walipoenda kuchukua mwili huo, umma ulihusisha watu wawili ambao waliwashutumu kwa kuhusika na shambulio la nyumba ya Bw Nyabuto.
Umati huo ulighadhabika na kutaka kuua washukiwa hao. Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani kutawanya umati huo uliokuwa na ghadhabu.
Polisi pia waliwarushia vitoa machozi kuwatawanya.
“Washukiwa hao wawili ni Bw Henry Bogecho, 22, na Edward Mogire, 25. Hatujui ni nini kilisababisha shambulio hilo lakini kesi hiyo inachunguzwa na makachero wetu wa upelelezi, (DCI),” Mkuu huyo wa Polisi alielezea.
Washukiwa hao wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Nyangusu na uchunguzi utakapokamilika, watafikishwa mahakamani kulingana na Bw Kipkulei.
Kamanda huyo wa polisi aliongeza kuwa wananchi walifurusha polisi kwa mawe, jambo ambalo liliwafanya kujibu kwa kuwafyatulia risasi hewani ili kuwatisha.
Afisa mmoja alipata majeraha madogo kwenye kiganja chake cha mkono wa kulia.
Gari la polisi hao, lilivunjwa vioo vyake.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Nyamache ukisubiri uchunguzi.