• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Wazazi waendea vitabu vya vishorobani

Wazazi waendea vitabu vya vishorobani

NA CHARLES ONGADI

HUKU shule zikifunguliwa kote nchini, wazazi wengi Mombasa walionekana kukimbilia vitabu vya bei nafuu vinavyouzwa kandokando mwa barabara na katika vishoroba badala ya maduka makubwa ya kuuza vitabu.

Wafanyabiashara wa kuuza vitabu vilivyotumika katika ujia mrefu wa kuelekea uwanja wa Makadara, mkabala na Posta Kuu, walionekana wakiwahudumia wateja wao waliofika kutoka maeneo mbalimbali Mombasa kununua vitabu tofauti.

Baadhi ya wafanyabiashara hao walionekana wakiwahudumia wateja wao huku wakihakisha hakuna mteja anayekosa kitabu anachohitaji.

Baadhi ya wazazi waliozungumza na Taifa Leo walisema walifikia uamuzi wa kununua vitabu chakavu kutokana na hali yao mbaya kimfuko inayozidi kung’ata kwa sasa.

“Hapa unaweza kupunguziwa bei ya kitabu ama upate kwa bei nafuu tofauti na maduka rasmi ya kuuzia vitabu ambako huko bei haishikiki,” akasema Bw Johnson Kalama ambaye ni mkazi wa Bombolulu aliyefika mjini kumnunulia mwanawe vitabu kadhaa.

Wazazi wengi walionekana kununua vitabu aina ya Encyclopedia ya Gredi ya Kwanza hadi Gredi ya Nane, Biblia ya Revised Standard, na Good News kwa wanafunzi wa shule za upili na msingi na Kamusi ya Kiingereza ya Oxford Dictionary.

Kulingana na Bi Ann Wanjiru ambaye ni muuzaji wa vitabu vilivyotumika, baadhi ya wazazi wanawaletea vitabu vilivyotumika na kubadilisha na wasivyokuwa navyo kwa bei ya maelewano.

Bi Wanjiru anasema vitabu hivyo hasa ni vya wanafunzi wa chekechea viwango vya PP1 na PP2 wanavyoviuza tena kwa kati ya Sh200 hadi 250 tofauti na bei ya maduka makubwa ya kuuza vitabu ambapo huko, bei ni kati ya Sh350 hadi Sh400.

Bw John Waithaka aliye na kibanda cha vitabu vilivyotumika karibu na msikiti ulio mita chache na uwanja wa Makadara jijini humo, anasema kwa kipindi cha siku mbili zilizopita, amekuwa akiuza vitabu vipya vya gredi za Kwanza hadi Nane.

“Kulingana na mtaala mpya wa umilisi almaarufu CBC, hakuna vitabu vilivyotumika. Hapa tunawauzia wateja wetu vitabu vipya lakini kwa bei nzuri,” akasema Bw Waithaka anayeagiza vitabu vyake kutoka jijini Nairobi.

Aidha, Bw Waithaka anafichua kwamba anauza nakala ya Biblia iliyotumika kwa Sh1,000 huku Encyclopedia ya gredi 1-8 ikienda pia kwa Sh1,000 tofauti na baadhi ya maduka makubwa yanayouza kwa kati ya Sh1,200 hadi Sh1,500.

Licha ya wazazi kukimbilia vitabu vilivyotumia vinavyouzwa kandokando mwa barabara, wenye maduka makubwa ya kuuza vitabu pia walifaidi kwani wazazi walifika huko kununua vitabu vya kuandikia, kalamu na bidhaa nyingine zinazohitajika shuleni.

Ikumbukwe kwamba huwa kuna utata kuhusu uamuzi wa kununua vitabu vinavyouzwa vishorobani kwani huwa kuna malalamiko kwamba baadhi huwa vimeibwa kutoka kwa waliokuwa wamiliki halisi.

  • Tags

You can share this post!

Nitaanza kutoka na vibenten kwa jinsi mnavyonisema, atishia...

Kanisa msalabani: Mjadala wa mapadri kuoa waibuka tena...

T L