Habari Mseto

Wazee wa Agikuyu wasambaza chakula kwa waathiriwa eneo la Makongeni

May 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

WAZEE wa Agikuyu wamejitolea kusambaza chakula kwa watu walioathirika eneo la Makongeni, Thika, Kaunti ya Kiambu.

Wakiongozwa na kiongozi wao – Muthamaki – Bw Njoroge wa Karatu, walisema Ijumaa kwamba walipata malalamiko mengi kutoka kwa wakazi wa Makongeni kuwa kuna watu kadhaa ambao hawana chakula na walitaka usaidizi.

Wazee hao, alisema, walifanya kazi ya busara na kuwajali watu 90 ambao wako katika hali ngumu ya maisha.

“Baada ya kupata habari hizo tulifanya juhudi kuzuru eneo la Makongeni ili kuwasaidia waathiriwa hao,” alisema Bw Karatu.

Shughuli hiyo iliendeshwa nje ya Kanisa Katoliki la St Mulumba, Makongeni, Thika.

Padri mkuu wa kanisa hilo Peter Mburu aliwapongeza wazee hao kwa kuchukua jukumu la kuwasaidia wakazi wa Makongeni kwa kuwapa chakula.

Alisema wazee hao watazidi kubarikiwa na Mungu kwa kuonyesha ukarimu wao.

“Ninawashukuru sana wazee hawa kwa kuonyesha unyenyekevu wao na kuwajali watu wengine,” akasema Mburu.

Chakula kilichotolewa ni unga wa ugali ambapo walionufaika ni wale ambao hawana uwezo wa kujikimu.

Wazee hao walisema huo ni mwanzo wa mambo na hivyo wakaahidi kwamba wataendelea kujipanga na kusaidia watu wengi.

Wazee hao walisema kujitolea kwao hakumaanishi wanavyo kwa wingi, lakini ni kuonyesha utu.

Hatua hiyo ya wazee wa Agikuyu kujitolea kutoa chakula imepongezwa na wakazi wa Makongeni.

“Wazee hao wanastahili kubarikiwa kwa ukarimu wao. Hiyo imeonyesha wanawajali watu wote wanaopitia hali ngumu hasa wakati huu wa janga la Covid-19,” akasema Charles Maina, mkazi wa mtaa wa Makongeni.