Habari Mseto

Wazee walalamikia kamatakamata ya wakongwe wakibandikwa Mungiki 

February 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

WAZEE wa Jamii ya Agikuyu sasa wanalalamikia hatua ya maafisa wa kiusalama eneo la Mlima Kenya wakisema inaonekana kulenga hata wakongwe wakiwahusisha na kundi haramu la Mungiki.

Mwenyekiti wa baraza hilo Bw Wachira Kiago ameteta kwamba “kuna msukumo wa ajabu wa kukutana hata na wakongwe wa miaka 90 na kuwatia mbaroni kwa msingi kwamba ni wafuasi wa kundi haramu la Mungiki”.

Akiongea wikendi katika kikao na baraza lake kujadili suala hilo, alisema wanatiwa mbaroni hata wakiwa katika safari za kulipa mahari, kutakasa boma, hafla za kifamilia na pia katika maombi yao ya kitamaduni”.
Alisema angetaka kuelewa kilicho ndani ya fikira za maafisa hao kinachowasukuma kudhania wakongwe kupindukia kuwa hatari kwa usalama wa taifa na pia kijamii.
“Wakati wanatupa hizo hekaya za abunuwasi kuhusu Mungiki, huwa wanatwambia kwamba genge hilo lilijulikana kwa kukata watu vichwa na kuwaua, kutoza ushuru haramu katika sekta za kibiashara na pia kutishia kupindua serikali,” akasema.

Bw Kiago alitaka kujua jinsi wanawake wa miaka 90 na wengine wa miaka ya kuanzia 60 wanaweza kuwa na uwezo wa kutekeleza maovu hayo ya genge la Mungiki.

“Mimi kama mwenyekiti wa baraza hili heshimika siwezi nikawa wa kutetea ukora. Lakini nao pia maafisa wa kiusalama wasitekeleze kazi yao kwa njia inayoashiria kuishiwa na busara, uadilifu na uhalisia wa kimawazo,” akasema.