Wazee wanastahili kulindwa, asema Wainaina
Na LAWRENCE ONGARO
WAKONGWE ni watu muhimu katika jamii ambao wanastahili kuheshimiwa pakubwa.
Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, kwa ushirikiano na kampuni ya mikate ya Broadway Bakery LTD Thika, waliwafadhili wazee wapatao 400 kwa kuwapatia vyakula kama mikate, mafuta ya kupikia, sabuni, na miavuli.
“Kuna haja ya kila mara kuwajali wazee kwa sababu wanapobaki nyumbani peke yao, wanastahili kupata utulivu wa akili,” alisema Bw Wainaina.
Alisema shirika la Jungle Afya limekuwa mstari wa mbele kwa miaka 10 likiwajali wakongwe kwa kuwahudumia katika makazi zao.
“Kuna wahudumu wa afya ya umma ambao kazi yao kuu huwa ni kuwatembelea wazee vijijini kwa lengo la kuwapa matibabu na chakula inapohitajika,” alisema Bw Wainaina.
Aliyasema hayo mnamo Jumanne katika ukumbi wa Gymkhana Thika, alipokutana na wazee hao kwa lengo la kuwapa blanketi na vifaa muhimu vya kuwasaidia wakiwa nyumbani kwao.
Walikuwa pia wakiadhimisha Siku ya Wazee Duniani.
Aliitaka serikali ifanye juhudi kuona ya kwamba wazee wanapata bima ya bure ya afya ya NHIF ili waweze kupata matibabu wakati wowote bila malipo.
Alitoa mwito kwa watu wanaofanya kazi mjini kufanya hima kwa kuwatembelea wazazi wao vijijini ili wawe na utulivu nyoyoni mwao.
Alisema uchunguzi uliofanywa umebainisha kuwa wazee wengi huaga dunia kwa sababu ya kudhalilishwa na familia zao na kukosa chakula.
“Wazee wengi wakibaki kwenye maboma hushindwa hata kujifulia nguo zao na hata kufagia nyumba zao. Pamoja na hayo ni kwamba wao huwa na upweke na baadaye msongo wa mawazo halafu hupoteza maisha,” alisema mbunge huyo.
Alisema ni makosa makubwa sana kwa mzee kufarika kwa sababu ya kukosa chakula.
“Kila mmoja popote pale alipo anastahili kutilia maanani maisha ya wakongwe hao ambao bado wana muda mrefu wa kuishi duniani,” alifafanua.
Alisema iwapo serikali itafanya juhudi kuweka mikakati bora ya kuangalia maslahi ya wakongwe, bila shaka watakuwa katika maisha ya kutamanika katika siku zijazo.