Habari Mseto

Wazee wasema Bunyasi tosha ugavana wa Busia 2022

September 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

WAZEE wa jamii ya Bakhayo wamemwidhinisha Mbunge wa Nambale Dkt John Bunyasi kuwania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Busia kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Wakiongozwa na mzee Peter Mangeni, wakongwe hao walisema Dkt Bunyasi ni msomi na kiongozi anayejivunia rekodi ya kupigiwa mfano ya maendeleo atakayehakikisha fedha zinazotengewa ustawi wa kaunti hazifujwi.

“Kama wazee na wenyeji tumejitolea mia fil mia kumuunga mkono Dkt Bunyasi katika mbio za kusaka ugavana 2022. Usimamizi wa fedha za kaunti huhitaji mtaalam wala si mwanasiasa na anayetosha kuvaa viatu hivyo ni mgombeaji wetu,” akasema Mzee Mangeni.

Akipokea uungwaji huo, Dkt Bunyasi alifichua kwamba tayari amezuru maeneo bunge yote saba ya gatuzi la Busia na kuandaa mikutano miwilli mikubwa na wenyeji, mikutano iliyojenga msingi wa kampeni zake.

“Kutokana na kushabikiwa na wapiga kura wa Busia nimeamua kujitosa mzima mzima katika kiny’ang’anyiro cha kupigania kiti cha ugavana 2022. Nimegombea ubunge mara tatu na wapinzani wangu huwa wanaiga manifesto yangu ambayo nitaanza kuinadi kwa wapiga kura ila sitafichua mbinu zangu za kusaka kura kwa wapinzani ndipo niwaangushe vizuri,” akajishaua Dkt Bunyasi.

Aidha mbunge huyo wa chama cha ANC alipongeza kazi ya gavana wa sasa huku akiahidi kuchuja atakaofanya nao kazi akilenga kutimiza ajenda ya maendeleo kwa wakazi wa kaunti hiyo ya mpakani.