Wazee watishia kwenda kortini kupinga mpaka wa kaunti ndogo
Na ALEX NJERU
MZOZO umeibuka kati ya wazee wa jamii ya Chuka, Wizara ya Usalama wa Ndani, baadhi ya wanasiasa wa eneo hilo na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuhusu mpaka wa Kaunti ndogo za Chuka na Igambang’ombe.
Wazee hao wametishia kuelekea mahakamani kupinga mpaka wa maeneo hayo mawili na kusema kaunti mpya ndogo ya Igambang’ombe imeingia hadi Chuka.
Wakizungumza kwenye kikao cha wanahabari mjini Ndagani jana, kikundi cha wakazi waliojumuisha pia vijana na wanawake, kililaumu baadhi ya wanasiasa kwa kutaka kugawanya jamii ya Chuka kwa sababu zao za kisiasa.
Bw Isaac Mugo ambaye ni mwenyekiti wa kikundi hicho, alisema hawataunga mkono wala kukubali uundaji wa Kaunti Ndogo ya Igambang’ombe ukamilishwe rasmi kabla malalamishi yao kutatuliwa.
Wazee hao walizidi kusema suala hilo linaweza kusababisha ugomvi kati ya makabila mawili ya Tharaka na Chuka kama suala hilo halitatatuliwa kwa tahadhari.
“Kuna wanasiasa ambao wamegawanya jamii ya Chuka bila sisi kujulishwa kwa sababu mpaka mpya umesababisha hali ya kuchanganyikiwa na tunahofia inaweza kuleta vita,” akasema Bw Mugo.
Aliongeza kuwa wameandika barua kwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i na IEBC pamoja na wabunge wa eneo hilo, wakitaka kushauriana nao.
Wazee wa jamii ya Njuri Ncheke, Mabw Eustace Muturi na Gerishon Kabiti, walisema hawataruhusu wanasiasa kusababisha mgawanyiko wowote wa makabila ya eneo hilo kwa sababu za kisiasa.