Waziri aiomba radhi jamii ya Abasuba watoto wao kusomeshwa kwa Kijaluo
Na Ibrahim Oruko
WAZIRI wa Elimu Amina Mohamed ameomba msamaha jamii ya Abasuba, ambao wengi wao wanaishi katika Kaunti ya Homa Bay, kutokana na hatua ya walimu kufunza watoto wao (sio walio kwa picha) kwa kutumia lugha ya Kijaluo.
Jamii ya Abasuba iliwasilisha malalamishi kwa Seneti ikisema kuwa watoto wao wanaosoma madarasa ya chini wanafundishwa kwa kutumia lugha ya Kijaluo hivyo kukiuka haki zao.
Jamii hiyo ilishutumu Taasisi ya Ukuzaji Mitaala (KICD) ambayo ilitangaza kuwa kuanzia Januari mwaka ujao watoto Wasuba watafunzwa kwa kutumia Kijaluo kama lugha yao ya kiasili.
Walilalama kuwa hatua hiyo itaangamiza lugha ya Abasuba ambayo kwa sasa inatishiwa kumezwa na Kijaluo. “Naomba msamaha ikiwa nilifanya makosa. Wizara imejitolea kuhakikisha kuwa lugha za kiasili zinakuzwa katika shule za chekechea na madarasa ya chini katika shule za msingi,” akasema Bi Mohamed alipofika mbele ya kamati ya Seneti kuhusu Elimu inayoongozwa na Christopher Langat.
Malalamishi hayo yaliwasilishwa katika Seneti mnamo Juni, mwaka huu ambapo jamii hiyo ilisema kuwa imebaguliwa kwa muda mrefu na lugha yao huenda ikatoweka.
Jamii ya Abasuba ilitambuliwa rasmi kama moja ya kabila za Kenya kupitia Gazeti Rasmi la Serikali la 1994. Serikali pia ilibuni wilaya ya Suba baadaye.
Notisi ya serikali pia iliagiza Taasisi ya Elimu (KIE) ambayo sasa inafahamika kama KICD, kuchapisha vitabu na vifaa vya kufundishia wanafunzi kwa kutumia lugha hiyo.